1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wa 8 wamekufa kwa ajali ya moto DRC

Admin.WagnerD21 Agosti 2023

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo watu 8 wamekufa katika ajali ya moto iliyotokea katika kambi moja ya waathirika wa mafuriko ya hivi karibuni wilayani Kalehe.

https://p.dw.com/p/4VPln
DR Kongo | Trauerfeier in Goma
Picha: Zanem Nety Zaidi/DW

Kwa sasa inakadiriwa familia zaidi ya 300 hazina mahapa pa kukaa baada ya kupoteza kila kitu ndani ya moto huo. Mwandishi wetu wa Bukavu Mitima Delachance anaeleza zaidi.

Kwa mujibu wa mashuhuda mbalimbali, moto huo ulitoka kwenye kibanda ambacho chakula kilikuwa kikiandaliwa. Kambi hiyo ilijengwa na manusura walioponea chupuchupu kwenye mafuriko katika vijiji vya Bushushu na Nyamukubi mnamo mwezi wa Mei mwaka huu.

Kambi ilijengwa kwa mahema yaliofunikwa kwa nyasi.

Kambi yenyewe ilikuwa imejengwa kwa kutumia mahema yaliyofunikwa na nyasi. Kwa vile mahema hayo yalikuwa yamejengwa pachapacha, moto uliochochewa na upepo ulienea haraka na kuteketeza kambi nzima.

Ajali hiyo ya moto ilitokea ikifuatia ajali nyingine ya kambi iliyounguwa moto katika wilaya ya Fizi ambapo inakadiriwa kuwa makaazi zaidi ya elfu moja ya muda ya wakimbizi yaliteketea katika kambi Malekya ndani ya eneo la Balala kusini.

Sierikali ya DRC yaonesha masikitiko.

DR Kongo | Trauerfeier in Goma
Baadhi wa waathirika wa mafuriko katika kambi ya Kalehe huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Picha: Zanem Nety Zaidi/DW

Serikali kuu mjini Kinshasa imeeleza masikitiko yake kufuatia matukio hayo yote. Kiongozi wa itifaki ya gavana wa Kivu kusini, Profesa Mubalama Zibona, amefanya ziara eneo la tukio ili kuwafariji waathirika.

Profesa Mubalama alisema kwamba serikali ya jimbo la Kivu Kusini kwa ushirikiano na mashirika ya misaada ya kiutu imechukuwa hatua zote ili waathirika wasiishi tena ndani ya mahema

Soma zaidi:Idadi ya waliouawa na mafuriko DRC yapita watu 400

Asasi za kiraia katika wilaya za Fizi na Kalehe zinatoa wito kwa serikali ya Kongo na mashirika ya misaada ya kiutu kuleta misaada kwa mara nyingine kwa waathirika hao, zikiitaka pia serikali kutimiza wajibu wake wa kuwalinda na kuwapatia waathirika makaazi hasa wakati huu kunapoandaliwa mwaka mpya wa shule.

Makadiro ya watu 18 wamepoteza maisha.

Idara ya Huduma ya Zimamoto ya Kivu Kusini inakadiria watu 18 wamepoteza maisha katika ajali za moto mjini Bukavu tangu mnamo mwezi Aprili mwaka huu.

Haya yanajiri wanati ambapo mjini Bukavu binti mwenye umri wa miaka kumi na saba amechomwa moto akiwa hai katika eneo la Mulungulungu kwa tuhuma kwamba ndiye chanzo cha ajali ya moto iliyoteketeza mamia ya nyumba eneo hilo kumepita wiki moja. Shirika la raia wa Mudusa limekemea kitendo hicho likitaka wanaohusika na mauaji hayo wawajibishwe mbele ya sheria.

DW Bukavu