Watu wa Bara la Afrika wapo hatarini kuambukizwa corona
26 Agosti 2021Bara la Afrika, limeshuhudia ongezeko la maambukizi mapya 248,000 ya COVID19, huku mataifa 28 yakishuhudia ongezeko la maambukizi ya corona hasa kirusi kipya cha Delta. Mkurugenzi wa shirika la afya duniani kanda ya Afrika, Matshidiso Moeti amesema hili ni janga linaloweza kuepukika iwapo mataifa ya Afrika yatapata na kufikia kwa usawa chanjo za COVID 19.
Moeti amesema milioni 13 ya chanjo ilifikishwa barani humo wiki iliyopita na hiyo ni mara tatu kuliko chanjo ilizipokea wiki zilizopita kama msaada kutoka kwa mataifa yalioendelea. Lakini idadi hiyo ni kidogo sana ukizingatia bara hilo lina takriban watu bilioni 1.3 ambapo kituo cha kudhibiti na kuzuwia magonjwa barani Afrika CDC kimesema kwa sasa asilimia 2.4 ya watu katika bara hilo ndio waliopewa chanjo.
Makali ya corona hasa kutokana na kirusi cha delta, inaendelea kuulemea mfumo wa afya barani Afrika. Lakini huku mataifa ya Afrika yakihangaika kupamabana na maambukizi ya corona, Marekani na mataifa mengine yalio na uchumi mkubwa wanazungumzia uwezekano wa kuwa na chanjo za nyongeza.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Afya Ulimwenguni Tedros Adhanom Ghebreyesus hivi karibuni amesema kuwa haipendezi kwa mataifa mengine kuanza kutoa chanjo za nyongeza wakati watu wengi zaidi bado hawajalindwa kutokana na ugonjwa wa COVID 19.
Moeti kwa upande wake amesema itakuwa vigumu kwa Afrika kuzungumzia chanjo hizo za nyongeza wakati hata asilimia 5 ya watu katika bara hilo hawajalindwa na chanjo inayohitajika kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo, na muhimu kuzuwiya kile wanachofikiria ni wimbi la nne la corona.
Marekani huenda ikaidhinisha chanjo ya Nyongeza
Wakati huo huo Marekani huenda ikaidhinisha chanjo ya tatu ya COVID 19 kwa watu wazima itakayotolewa miezi sita baada ya kupokea chanjo ya kwanza na ya pili badala ya ilivyotangazwa hapo awali kuwa muda wa kusubiri chanjo ya tatu utakuwa miezi minane.
soma zaidi: Afrika yakabiliwa na wimbi la 3 la corona
Kuidhinishwa kwa chanjo hiyo ya tatu itakayotengenezwa na kampuni ya Pfizer na kampuni shirika ya BioNTech SE, Moderna Inc na Johnson & Johnson kunatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, hii ikiwa ni kwa mujibu wa jarida la Wall Street Journal likimnukuu mtu aliyekuwa karibu na mipoango hiyo.
Nchini Austaralia maambukizi mapya ya COVID 19 yamefikia 1000 hii leo kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa janga la corona huku hospitali mbili kubwa mjini Sydney zikiweka kambi nje ya hospitali kupambana na ongezeko la wagonjwa.
Mkuu wa jimbo la New South Wales Gladys Berejiklian amesema eneo lake limeongeza idadi ya vifaa vya kutolea Oksijeni.
Amesema licha ya mfumo wa afya kuanza kudizidiwa wanaweza kudhiti hali ilivyo kwa sasa pindi idadi ya watu waliochanja itakapopanda.
Chanzo: ap/reuters