Watu wanajiuliza: Vipi itakuwa Cuba bila ya Fidel Castro?
3 Agosti 2006Tangu habari hiyo kugonga vichwa vya habari, watu wamekuwa wakijiuliza: Cuba itaelekea wapi pindi kiongozi huyo atafariki dunia?
Alipoulizwa na waandishi wa habari wiki moja iliopita juu ya tetesi zilizoenea wakati huo kwamba hatoishi siku nyingi, Fidel Castro alisema, na hapa ninamnukuu: Karibu kila siku mimi nakufa, jambo hilo linanipa raha, na kutokana na hali hiyo ninakuwa zaidi mwenye afya.+
Wa-Cuba walio uhamishoni huko Miami, Marekani, serekali yenyewe ya Marekani, wapinzani wa Cuba na watu wengi wengine watatosheka pindi Fidel Castro ataaga dunia. Kwa miaka watu hao wamekuwa wakifikiria kwamba kifo cha kawaida cha kiongozi huyo wa Cuba kitakuwa ni suluhisho kwao. Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi aliye madarakani kwa muda mrefu kabisa kuliko yeyote duniani na mwanamapinduzi mzee kabisa aliye madarakani hapa duniani sio kwamba hatokufa.
Baadhi ya watu wanaona kufariki dunia Castro kutafungua njia kwa Cuba kuwa na mwanzo mpya. Utawala wa Castro, miaka 47 sasa tangu ushike madaraka, miaka 15 tangu kumalizika Vita baridi baina ya kambi za Mashariki na Magharibi na kusambaratika Urussi, umejizatiti barabara. Kwa upande mwengine, yale matarajio kwamba kutakuweko mwanzo mpya kabisa huko Cuba ni sawa na kuota. Kuelemea idadi zaidi ya nchi za Amerika ya Kusini katika mrengo wa siasa za shoto kumeitoa Cuba kutoka ile kona ya uchafu, na sasa watu wanapendekeza kuweko na mdahalo na utawala huo wa kikoministi. Uruguay na Argentina katika miaka ya karibuni zimeanzisha uhusiano wa kibalozi na Cuba. Wiki chache zilizopita, Fidel Castro alikuwa mgeni katika mkutano wa kilele wa nchi za Amerika ya Kusini.
Hakuna cha kuficha na kujidai mambo ni mazuri. Huko Cuba kuna utawala wa mabavu. Kwa mujibu wa jumuiya za kupigania haki za binadamu, zaidi ya wapinzani 300 wako vizuizini kama wafungwa wa kisiasa. Hali ya kiuchumi katika nchi hiyo ilioko katika Bahari ya Karibian ni mbaya, na ni tu kupitia rushwa na kuhonga ndipo wanapoweza wananchi wa Cuba kujipatia mahitaji muhimu ya kila siku. Utalii, ambao ndio njia ya pili kubwa kwa nchi hiyo kujipatia fedha za kigeni, umeifanya jamii ya Cuba igawike katika tabaka mbili, jambo linaloifanya kuwa ni upuuzi ile fikra ya kujenga ujamaa katika nchi hiyo. Watu wanachunguzwa nyendo zao kupitia zile zinazoitwa kamati za mapinduzi za mitaa. Mapinduzi hayo ya Cuba haiyawaamini kabisa wananchi wake wenyewe. Kwa hakika utawala wa Castro umepitwa na wakati kabisa kuweza kutoweka kwa heshima.
Katika kipindi cha mpito kitakachokuwa cha nidhamu, angalau, itawezekana mambo mengi ya hivi sasa kuhusu huduma za jamii kuyaingiza katika enzi mpya. Hata ile tume ya haki za binadamu na upatanishi wa taifa ambayo inaulaumu sana utawala wa sasa inakiri juu ya ubora wa huduma za kijamii za Cuba, ukilinganisha na nchi nyingine za Amerik ya Kusini. Kutokana na huduma nzuri kisiwani humo, Wa-Cuba wanaishi sasa hadi umri mkubwa kabisa na ni idadi ndogo sana na watoto wachache wanakufa.
Licha ya ukandamizi na matatizo ya kiuchumi yalioko huko Cuba, wananchi wa huko hawataki Wamarekani au Wa-Cuba walioko uhamishoni huko Miami waende huko kama wakombozi wao.. Wanaashiria kwamba wanajeshi wa Kimarekani walipokwenda Iraq baada ya kupinduliwa Saadam Hussein hawajakumbatiwa na kusheherekewa kama wakombozi.
Na kumbuka kwamba baada ya kuanguka Ukuta wa Berlin na kupotea ile iliokuwa inaitwa Jamhuri ya Kidimokrasi ya Ujerumani, DDR, wakaazi wa mikoa ya hiyo iliokuwa Ujerumani Mashariki walikataa kuambiwa nini cha kufanya na wakaazi wa Ujerumani magharibi. Wao kwa miaka 40 waliishi katika upande ulioshindwa ndani ya historia. Asilimia 70 ya Wa-Cuba wamezaliwa baada ya mapinduzi, wanaijua nchi yao tu chini ya uongozi wa Fidel Castro. Na wanaipenda nchi yao, licha ya kuweko Castro. Jambo hilo lisidharauliwe, itakuwa vivyo hivyo hata katika enzi ya Fidel na ndugu yake, Raul.