1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 500 wauawa Nigeria

8 Machi 2010

Nchini Nigeria kiasi cha watu 500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa kufuatia kuibuka kwa mapigano mapya ya kidini jana Jumapili katika kijiji cha Dogo, karibu na mji wa Jos.

https://p.dw.com/p/MMoV
Askari wa Nigeria akidhibiti usalama katika mji wa JosPicha: AP

Kwa mujibu wa watu waliyoshuhudia mauaji hayo, washambuliaji waliwazingira wanakijiji, katika shambulio linaloonekana kuandaliwa vyema.

Afisa mmoja wa serikali aliyekataa kutaja jina lake ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kuwa takriban watu 500 wameuawa katika shambulio hilo, na kuongeza kuwa wengi wa waliyouawa ni wanawake na watoto waliyo chini ya umri wa mwaka mmoja.

Kijiji cha Dogo Nahawa kilichoko karibu na mji wa Jos kilizingirwa na washambuliaji hao, kabla ya wakaazi wake kushambuliwa.Pia walichoma moto nyumba katika vijiji vya Ratsat naZot vilivyoko kiasi ya kilomita 10 kutoka Jos, vijiji ambavyo hukaliwa na watu wa kabila la Berom.

Dan Azumi ambaye ni kiongozi wa kijiji hicho cha Dogo Nahuwa amesema

´´Watu saba kutoka famaili yangu pekee wameuawa.Watu wengi sana wameuawa katika kijiji, na watu hawa waliyotushambulia´´

David Daniel David mkazi wa kijiji cha Ratsat ameliambia shirika hilo la habari la Ufaransa kuwa watu waliyotekeleza mauaji hayo ni wa kabila la Fulani.Pia makundi ya wanaharakati wa haki za binaadamu katika mji huo wanawalaumu watu wa kabila la Fulani kuhusika na shambulio hilo.

Peter Gyang ambaye mke wake pamoja na watoto wawili ni miongoni mwa waliyouawa, amesema mauaji hayo yalianza mnamo milango ya saa 3 asubuhi kwa saa za Nigeria na kuendelea hadi saa 12 jioni, na kwamba hakukuwa na milio yoyote ya risasi.Kwa muda wote huo anasema hakuna askari polisi hata mmoja aliyefika.

Dolop Mencher ni mbunge kutoka eneo la kusini mwa Jos ambaye alishuhudia mauaji hayo.

´´Nimeshuhudia tukio la unyama wa hali juu na la kutisha, kwa kweli siyo tukio la kibinaadam kabisa.Shambulio hili liliandaliwa kwa ustaadi wa hali juu.Nimeona maiti zaidi ya 30´´

Mjini Jos, Yusuf Alkali ambaye ni kutoka kabila la Fulani amesema kuwa anaamini shambulio hilo ni ulipizaji kisasi kufuatia kuuwa kwa viongozi wanne wa kabila hilo la Fulani na vijana wa kabila la Berom mnamo wiki mbili zilizopita.

January mwaka huu, zaidi ya watu 300 waliuawa katika ghasia za kidini zilizotokea kwenye mji huo huo wa Jos, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Plateau lililoko katikati ya Nigeria.

Kaimu Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameamrishwa kupelekwa askari zaidi, kuimarisha usalama kwenye jimbo hilo.

Pia ameagiza vikosi vya usalama kuanzisha mkakati maalum wa kudhibiti na kuwakamata wahusika wa ghasia hizo. Dan Manjang, ambaye ni mshauri wa gavana wa jimbo la Plateau amethibitisha kuwa majeshi yamekwishapelekwa kwenye eneo la tukio.

Kwa upande mwengine mwandishi wa DW idhaa ya kihausa mjini Lagos, anaarifu kuwa marais saba wa zamani wa Nigeria, wanakutana mchana huu mjini Jos na magavana wa majimbo saba, nchini humo, kujadiliana juu ya mapigano hayo ya kidini ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwenye jimbo hilo la Plateau.

Mbali ya tukio la January mwaka huu, Novemba mwaka 2008, zaidi ya watu 200 waliuawa kufuatia mapigano kati ya waumini wa dini hizo mbili, yaliyosababishwa na matokeo ya uchaguzi katika mji wa Jos.Shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Human Right Watch linasema idadi ya watu waliyouawa katika ghasia hizo ni zaidi ya 700.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Othman Miradji