Watuhumiwa wa uhujumu wa uchumi Tanzania waomba msamaha
30 Septemba 2019Watu 467 ambao wameshtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi nchini Tanzania wameandika barua wakiomba msamaha kama ilivyoshauriwa na rais wa taifa hilo John Magufuli ambaye alitaka wale watakaokiri makosa yao na kukubali kulipa fedha waruhusiwe kurejea uraiani.
Washtakiwa hao walioko gerezani wametumia fursa hiyo kama ilivyoshauriwa na Rais Magufuli wiki moja iliyopita na kwamba wanatarajia kurejea uraiani muda wowote kuanzia sasa baada ya kukamilisha taratibu za kisheria.
Akizungumza ikulu baada ya kupokea taarifa ya mkurugenzi wa mashtaka, Rais Magufili amesema msamaha huo aliotoa haimainisha kwamba amefungua milango kwa watu kujitumbukiza kwenye makosa ya uhujumu uchumi.
Washtakiwa hao ambao makosa yao waliyafanya kwa nyakati tofauti wanatarajia kulipa kiasi cha shilingi Bilioni 107.8 kiwango ambacho kitalipwa kwa mkupuo na kwa awamu kadhaa.
Kuachiwa kwa washtakiwa hao kunafungamana na sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyopitishwa septemba mwaka huu inayotoa ruksa ya kufanyika mapatano baina ya watuhumiwa na mwendesha mashtaka.
Sheria hiyo inasema kuwa yeyote kati ya mtuhumiwa, wakili wake ama mwendesha mashtaka anaweza kuanzisha mapatano kwa kuiarifu mahakama.
Katika makubaliano hayo, mtuhumiwa anaweza kukiri tuhuma ama sehemu ya tuhuma dhidi yake ili kupata afueni fulani ikiwemo kuondolewa baadhi ya mashtaka,ama kupunguziwa muda ama aina ya adhabu.
Pamoja na kupokea taarifa ya wale waliokiri makosa yao, kadhalika Rais Magufuli ametoa muda mwingine wa siku saba kwa washtakiwa wengine ambao walikuwa bado hawajafikia uamuzi wa kuomba msamaha.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mashtaka ya uhujumu uchumi hayana dhamana, na wote wanaoshtakiwa kwa makosa hayo husalia rumande mpaka hukumu zao zinapotolewa.
Tangu aingie madarakani miaka minne iliyopita Rais Magufuli amekuwa akijipambanua kama kiongozi anayekabiliana na rushwa na ufisadi. Chini ya utawala wake vigogo kadhaa wameshuhudiwa wakitiwa korokoroni kwa makosa yanayohusiana na uhujumu uchumi na utakakatishaji fedha.
Baadhi ya watu mashuhuri wanaokabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi ni mwanahabari wa uchunguzi Erick Kabendera, aliyekuwa kamishna wa mamlaka ya mapato, Harru Kitilya na waliokuwa vigogo wa shirikisho la soka TFF.