Waturuki wapiga kura ya kumpa Rais madaraka zaidi au la
16 Aprili 2017Iwapo kambi ya Erdogan itashinda, basi huenda akasalia madarakani hadi mwaka 2029. Upinzani unasema kumuongezea Rais mamlaka ni hatua kuelekea utawala wa kiimla. Matokeo hayo pia yataamua mustakabali wa uhusiano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya.
Taifa hilo ambalo ni mwanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO imechangia katika kupunguza mmiminiko wa wakimbizi katika nchi za Umoja wa Ulaya baada ya kufikia makubaliano kati ya Uturuki na Umoja huo. Hata hivyo kutokana na kuzorota kwa uhusiano kati ya pande hizo mbili, Rais Erdogan amasema atatathmini upya makubaliano hayo baada ya kura ya maoni.
Upinzani wasema madaraka zaidi ni udikteta
Zaidi ya Waturuki milioni 55.3 wamesajiliwa kupiga kura huku wale walioko katika nchi za kigeni wakiwa tayari wameshapiga kura kabla ya kura hiyo ya leo ambayo iwapo itakubalika itampa Erdogan madaraka makubwa kuliko kiongozi mwingine yule Uturuki tangu muasisi wa taifa hilo Mustafa Kemal Ataturk na aliyefuata Ismet Inonu.
Wachambuzi wanasema matokeo ya kura hiyo hayaweza kutabirika bayana licha ya kambi ya ndiyo kuwa na raslimali nyingi na muda wa kutosha katika vyombo vya habari kunadi kampeini zao. Kambi ya upinzani ilifanya kampeini kabambe hadi dakika za mwisho Jumamosi kuwashawishi wapiga kura amabo hawajaamua watapiga upande gani. Erdogan amesema ana imani kambi ya ndiyo itanyakua ushindi.
Iwapo Waturuki wataamua kumpa rasi madaraka, mfumo huo mpya wa uongozi utaanza kufanya kazi baada ya chaguzi kuu za Novemba 2019, Erdogan ambaye alichaguliwa rais mwaka 2014 baada ya kuhudumu kama Waziri mkuu kuanzia 2003 huenda akagombea mihula mingine miwili ya miaka mitano kila mmoja.
Kura hiyo itakuwa na athari kubwa katika mchakato wa taifa hilo kujiunga na Umoja wa Ulaya. Rais huyo wa Uturuki ameonya kuwa iwapo atashinda katika kura hiyo ya maini atatia saini mswada wowote utakaokubalika na bunge wa kurejesha adhabu ya kifo, hatua ambayo moja kwa moja itasitisha mchakato wa nchi hiyo kujiunga na Umoja huo.
Vituo vya kupigia kura vinafunguliwa saa moja asubuhi na kutarajiwa kufungwa jioni. Usalama umeimarishwa maradufu baada ya nchi hiyo kukumbwa na misururu ya mashambulizi ya kigaidi. Zaidi ya polisi 33,500 watashika doria mjini Istanbul pekee siku hii ya kura ya maoni.
Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo