Raia zaidi ya milioni mbili wakimbia mapigano Ukraine
8 Machi 2022Raia kutoka mji moja wa mashariki mwa Ukraine walikuwa wanaondoka kwa kutumia mabasi siku ya Jumanne, kufuatia usitishaji mapigano katika eneo hilo, baada ya Urusi na Ukraine kukubaliana kuweka njia salaama kwa ajili ya watu wanaotoroka mapingano.
Urusi ilikubali kuweka "njia za kibinadamu" kutoka miji minne katika siku ya 13 ya vita, licha ya Umoja wa Mataifa kusema idadi ya wakimbizi wanaofurika katika mipaka ya Ukraine imepita milioni mbili.
Lakini Ukraine iliishutumu Urusi kwa kushambulia njia nyingine inayotoka katika mji wa bandari wa kusini wa Mariupol, ambapo wafanyakazi wa misaada walisema makumi kwa maelfu walikuwa wakiishi katika mazingira ya vurugu.
Kyiv imezitaja njia za miji minne kuwa ni za geresha tu kwani njia nyingi za kutokea zinaelekea Urusi au mshirika wake Belarus. Pande zote mbili zinashutumiana kwa ukiukaji wa usitishaji mapigano.
Mzozo mkubwa wa wakimbizi
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umezusha hofu ya mzozo mkubwa wa Ulaya au hata wa kimataifa, na kuibua mgogoro wa wakimbizi unaokua kwa kasi zaidi barani humo tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Vikwazo vikubwa vya kimataifa vimeshindwa kumshawishi Putin arudi nyuma, na hivyo kusababisha mataifa ya Magharibi kuzingatia vikwazo vya nishati licha ya uwezekano wa maumivu pia kwa uchumi wao.
Bei ghafi zilipanda baada ya Ikulu ya White House kusema Biden atazungumza JUmanne "kutangaza hatua za kuendelea kuiwajibisha Urusi kwa vita vyake visivyo na msingi na visivyo vya haki dhidi ya Ukraine".
Wanajeshi wa Urusi wanaisogelea Kyiv polepole licha ya juhudi kubwa za vikosi vya Ukraine vilivyozidiwa, na kusonga kwa kasi mashariki na kaskazini mwa nchi.
Soma pia: Wanajeshi 70 wa Ukraine wauwawa
Licha ya sauti za makombora kwenye mji wa karibu wa Irpin, unaoonekana kama kituo muhimu cha kusonga mbele kuelekea mji mkuu, raia walikimbia katika upepo wa barafu na theluji kubwa, waandishi wa habari wa AFP walishuhudia.
Watu walisubiri kwenye mstari mrefu ili kuvuka mto Irpin kwenye njia za muda za mbao na chuma zilizochongwa, baada ya Waukraine kulipua daraja linaloingia mji mkuu ili kuzuia kusonga mbele kwa majeshi ya Urusi.
"Sikutaka kuondoka, lakini hakuna mtu aliyesalia katika nyumba zilizo karibu nasi, hakuna maji, hakuna gesi na hakuna umeme," Larissa Prokopets, 43, aliiambia AFP.
Alisema alikuwa akiondoka baada ya kukaa kwa siku kadhaa "mafichoni ya chini" ya nyumba yake, ambayo iliendelea "kutikisika" kutokana na mashambulizi ya mabomu karibu.
Soma pia: Serikali za Afrika zaanza kuhangaika kuondoa raia wao Ukraine
Urusi ilikuwa imekataa wito wa kuwepo kwa ukanda wa kibinadamu mjini Irpin na vitongoji vya karibu vya Bucha na Gostomel "ingawa tulikuwa tumetayarisha na kila kitu kwa hili," afisa wa wizara ya mambo ya ndani wa Ukraine Anton Gerashchenko alisema.
Hata hivyo uhamishaji ulikuwa umeanza Sumy, karibu na mpaka wa Urusi na umbali wa kilomita 350 (maili 218) mashariki mwa Kyiv, ambapo Urusi ilikuwa imetangaza rasmi ukanda wa kibinadamu, maafisa walisema.
Makumi ya mabasi tayari yalikuwa yameondoka kuelekea Lokhvytsia, kusini magharibi, alisema kaimu gavana wa mkoa wa Poltava, Dmitry Lunin. Ukanda huo umeundwa kuwaondoa raia, wakiwemo Wachina, Wahindi na wageni wengine, maafisa walisema.
Uhamisho huo ulikuja baada ya watu 21, wakiwemo watoto wawili, kuuawa mkoani Sumy wakati "ndege za adui ziliposhambulia kwa hila majengo ya ghorofa," ilisema idara ya huduma za uokoaji ya Ukraine.
Watu watatu waliuawa na watoto watatu kujeruhiwa na bomu la kutegwa ardhini mjini Chernihiv, kaskazini mwa Kiev, maafisa walisema.
Athari za kiuchumi za mzozo
Athari za kiuchumi za mzozo huo, unaohusisha msafirishaji wa juu wa nishati ya gesi na mafuta duniani, umechochea wasiwasi kwamba unaweza kuchelewesha ufufuaji wa uchumi wa dunia kutokana na janga la virusi vya corona.
Moscow inazitaja hatua zake nchini Ukraine kama "Operesheni Maalumu" ya kumvunja nguvu jirani yake na kuondoa viongozi inaowataja kuwa wanazi-mamboleo.
Ukraine na washirika wake wa magahribi wanakiita hiki kuwa kisingizio kisicho na msingi kuhalalisha uvamizi ili kuiteka nchi hiyo yenye wakaazi milioni 44.
Soma pia: Marekani au Urusi? Mzozo wa Ukraine waiweka njia panda Ghuba
Vikwazo vya mataifa ya magharibi vimeifungia Urusi nje ya mfumo wa kimataifa wa fedha na masoko kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa dhidi ya taifa lenye uchumi mkubwa kama huo, huku mapigano kusini mwa Ukraine yakizuwia mauzo yake ya nje kwa sehemu kubwa.
Ukraine inasema kasi ya kusonga mbele kwa vikosi vya Urusi imepungua Jumanne, huku wizara ya ulinzi ya nchi hiyo ikitangaza kwamba Meja Jenerali wa Urusi, Vitaly Gerasimov, ambaye ni naibu kamanda wa kwanza wa kikosi cha 41 cha jeshi la Urusi, aliuawa jana Jumatatu, akiwa ni meja jenerali wa pili wa Urusi kuuawa tangu kuanza kwa uvamizi. Wizara ya Ulinzi y aurusi haikupatika mara moja kutoa kauli.
Urusi ilidharau upinzani wa Ukraine, afisa wa Marekani anasema
Afisa mkuu wa ujasusi wa Rais Joe Biden alisema Jumanne kwamba Marekani inaamini kuwa Urusi ilidharau nguvu ya upinzani wa Ukraine kabla ya kuanzisha uvamizi ambao huenda umesababisha maelfu ya Warusi kupoteza maisha.
Mkurugenzi wa Idara ya ujasusi wa kitaifa Avril Haines aliliambia jopo la wabunge kwamba maafisa wa Marekani wanaamini kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin anahisi ``kusikitishwa'' na kushindwa kwa Urusi kuitiisha Ukraine na kwamba anaona kwamba hawezi kumudu kushindwa vitani.
Soma pia: Biden: Putin alijidanganya anaweza kusambaratisha NATO
Lakini kile ambacho Putin anaweza kufikiria kuwa ushindi kinaweza kubadilika kutokana na kuongezeka kwa gharama za mzozo kwa Urusi, Haines alisema.
Licha ya tangazo la Putin kwamba angeongeza kiwango cha tahadhari ya silaha za nyuklia za Urusi, Haines amesema Marekani haijaona mabadiliko yasiyo ya kawaida katika mkao wa nguvu ya nyuklia ya Urusi.
Haines alisema ``haijulikani katika hatua hii'' ikiwa Urusi itajaribu kuiteka Ukrainia yote, jambo ambalo lingehitaji rasilimali zaidi kuliko ambavyo Putin ameahidi.
Viongozi wakuu wa mataifa ya Marekani, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, wamekubaliana kuendelea kupandisha gharama kwa Urusi, na kutilia mkazo dhamira yao ya kutoa msaada wa kiusalama, kiuchumi na kibinadamu kwa Ukraine, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ikulu ya White House baada ya mkutano wao wa vidio.
Chanzo: Mashirika