1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wavuvi wa Ufaransa waandamana dhidi ya hatua za Uingereza

Saleh Mwanamilongo
6 Mei 2021

Meli za kivita za Uingereza na Ufaransa zimepiga doria kwenye kisiwa cha Jersey, kufuatia maandamano ya baharini ya meli za wavuvi wa Ufaransa.

https://p.dw.com/p/3t46U
Saint Helier | Französische Fischer blockieren Hafen von Jersey
Picha: Josh Dearing/PA/picture alliance

Wavuvi wenye ghadhabu kutoka Ufaransa waliingia kwenye bandari ya Jersey, katika hali inayoashiria mzozo mkubwa baina ya Ufaransa na Uingereza kuhusu haki ya uvuvi baada ya Brexit. Umoja wa Ulaya umetowa wito wa utulivu,  huku ukiishutumu Uingereza kwa kutoheshimu mkataba wa kibiashara uliotiwa saini baina ya pande hizo mbili baada ya mchakato wa Brexit.

 Viongozi wa Ufaransa walifahamisha mapema leo kuwa meli mbili za polisi wa baharini zilipelekwa kwenye maji ya Ufaransa na kisiwa cha Jersey. Hatua hiyo inafuatia ile ya Uingereza ya kupeleka jumatano meli zake mbili za kivita kwenye eneo hilo, la bahari ya kaskazini.

''Kwetu sisi ni masharti ya upuuzi''

Wavuvi wa Ufaransa waliandamana na meli zao kwenye maji ya kisiwa cha Uingereza cha Jersey, ilikupinga kanuni mpya za uvuvi zilizowekwa na Uingereza kufuatia Brexit. Kanuni hizo ni pamoja na kuwataka wavuvi hao kuwasilisha rekodi yao ya uvuvi kabla ya kupewa leseni ya kuendesha shughuli kwenye maji hayo. Hugo Lehuby,mkuu wa kamati ya wavuvi wa Ufaransa amesema wamechoshwa na masharti yaliowekwa na Uingereza.

''Tunaandamana kwa sababu ya kero kuhusu leseni za uvuvi ambazo zinamasharti mengi sana na ambazo ni tofauti na wenzetu wa Uingereza. Masharti hayo yamewekwa kinyume cha sheria na yamekiuka mkataba wa Brexit. Kwetu sisi ni masharti ya upuuzi'',alisema Lehuby.

Wavuvi wa Ufaransa wamesema baadhi ya meli zilizokuwa zikifanya kazi kwa muda mrefu kwenye maji hayo, zilitakiwa kusitisha shughuli hizo.

Brexit na suala tete la uvuvi

Frankreich Fischerprotest in Calais
Picha: Getty Images/AFP/P. Huguen

Dimitri Rogoff, anayeongoza kundi la wavuvi kutoka Normandie, kaskazini magharibi mwa Ufaransa, amesema takriban meli hamsini ziliandamana leo alhamisi kwenye bandari ya kisiwa cha Jersey, St-Helier. Rogoff amesema maandamano hayo kuhusu leseni za uvuvi sio jaribio la kuzuwiya shughuli kwenye bandari ya Jersey. Ufaransa ilifahamisha kuwa meli zake za polisi zipo hapo kwa ajili ya usaidizi wowote wa dharura.

Kwa upande wake serikali ya Uingereza imesema meli zake za kivita zitaendelea kubaki hapo kuangalia hali ilivyo kama hatua ya tahadhari. Waziri mkuu wa Uingereza Boris Jonson amekosolewa na upinzani kwa kuchochea mzozo huo, akitumia suala hilo kama kitu cha kuvutia siku ya uchaguzi.

Makubaliano ya Brexit yasiyokuwa na ushuru kwa bidhaa kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza yalianza kutekelezwa Januari, wakati miezi tisa ya mpito baada ya mchakato wa Brexit ilipokamilika. Lakini mkataba huo unajumuisha pia suala tete la uvuvi.