Wazambia wamchagua Rais mpya
12 Agosti 2016Rais wa Zambia Edgar Lungu na mpinzani wake mkuu Hakainde Hichilema wote wamesema wana imani wataibuka washindi katika uchaguzi huo. Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa kumi na mbili asubuhi huku milolongo mirefu ya watu ikishuhudiwa katika vituo hivyo.
Baada ya kukamilika kwa kipindi cha kampeni kilichoghubikwa na vurugu, Lungu na Hichilema waliwatolea wito wapiga kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura kila mmoja akiahidi kuuimarisha uchumi wa taifa hilo ambao unasuasua.
Wafuasi wa chama tawala PF na wa UPND walikabiliana wakati wa kampeini na kusababisha hata tume ya uchaguzi kusitisha kampeini hizo kwa muda.
Upande wa upinzani umekuwa ukisumbuliwa
Wazambia wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira baada ya kufungwa kwa migodi ya madini ya shaba, kupotea mara kwa mara kwa umeme na kupanda kwa bei za vyakula na mahitaji ya kimsingi.
Mbali na kumchagua rais, wabunge na madiwani, raia wa Zambia pia wanapiga kura ya maoni ya kuifanyia mageuzi katiba ya nchi hiyo.
Mgombea urais atahitaji kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kuepusha duru ya pili ya uchaguzi, iwapo sivyo, duru hiyo ya pili itahitaji kufanyika katika kipindi cha siku 37 baada ya uchaguzi huu wa Alhamisi.
Matokeo kamili ya uchaguzi huo mkuu yanatarajiwa kutolewa siku ya Ijumaa au Jumamosi.
Nchi ya Zambia tofauti na nchi zingine za jirani kama vile Angola na Zimbabwe haijaingia katika vita na machafuko makubwa tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1964 ambapo mwaka 2011 kulifanyika uchaguzi wa amani ambao ulimuweka Michael Sata kuwa rais wa nchi hiyo mpaka mwaka 2014 alipofariki na mwaka 2015 kufanyika uchaguzi mwingine uliomuweka Edgar Lungu kuwa raisi wa nchi hiyo ili kumalizia muhula ulioachwa na Rais Sata.
Mara kwa mara Hichilema amekuwa akishutumiwa na maafisa kuwa anapuuzia mashambulizi ambayo yanafanywa na wafuasi wake na mara kadhaa amekamatwa na nyumba yake kuzingirwa na polisi.
Hali ya uchumi ni dhaifu
Chama hicho cha upinzani kinakishutumu chama cha PF kwa kushindwa kudhibiti msukosuko uliosababishwa na kuanguka kwa bei ya madini ya shaba ambayo ndio yenye kuzalisha pato kuu la taifa na ukame uliopelekea uhaba wa umeme mambo yaliosababisha kushuka thamani kwa sarafu ya kwacha na kupanda kwa gharama za maisha.
Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP
Mhariri: Caro Robi