Wazee walilia kutekelezwa na watoto wao
1 Oktoba 2018Pamoja na changamoto lukuki za kisera zinazowakabili wazee nchini Tanzania, wazee wilayani Kasulu mkoani Kigoma waliiambia DW kuwa wanaumizwa na tabia ya kutelekezwa na watoto sambamba na kuachiwa kulea wajukuu.
Bibi Cotrida Kokupima, kiongozi wa shirika la Saidia Wazee Tanzania (SAWATA) wilayani Kasulu linalofanya kazi na shirika la kimataifa la Help Age International, anasema pamoja na shida nyingine za kisera kuwabinya wazee, "vijana wengi wanawatelekeza wazazi wao katika umri wa uzee jambo ambalo lina athari kubwa."
Watu wengi, hasa vijana wanaotuhumiwa kuwaacha wazee na kwenda kuishi mijini, hudhani kuwa maisha magumu ya wazee yanatokana na uzembe wakati wa ujana wao, hasa kwa waliokuwa watumishi wa umma.
Lakini Mzee Jakson Lumenyera aliyekuwa mwalimu na baadaye mpiganaji katika vita vya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika anabainisha kuwa kipato cha mtumishi mwadilifu hakimpi fursa mfanyakazi kuweka akiba yoyote ya kuja kumfaa uzeeni, "vyenginevyo awe kwenye utumishi wake hakuwa mwadilifu."
Suala la kuwaandalia fursa vijana ili wawe walezi wa wazee linatajwa kukwama kutokana na vijana wengi badala ya kusaidiana na wazazi kujenga uchumi wa kaya zao huhujumu juhudi za wazazi wao, anasema Idd Mwicha kutoka Kasulu.
Kubwa zaidi kuna masuala mazima ya vijana kuhamia mijini na kusahau walikotoka kwa maana ya waliko wazazi wao, kuporomoka kwa maadili ya kijamii na maandalizi duni ya familia katika kutengeneza mfumo mzuri wa maisha ya baadaye kwa watoto. Bi Sanyu Jame Kihungu ameaimbia DW kuwa haya ndiyo chanzo cha wazee wengi kujikuta wakiishi katika upweke bila msaada wa watoto.
Maadhimisho ya siku ya wazee duniani hufanyika kila mwaka Oktoba Mosi, nchini Tanzania mwaka huu sherehe za wazee zilifanyika mjini Arusha kwa kauli mbiu isemayo "Wazee ni hazina ya Taifa, tuenzi juhudi za kutetea haki na ustawi wao."
Mwandishi: Prosper Kwigize/DW Kigoma
Mhariri: Josephat Charo