1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fabius aacha uwaziri

Admin.WagnerD10 Februari 2016

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amejiuzulu wadhifa huo . Bwana Fabius ambae pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu ameteuliwa kuwa Rais wa Baraza la Katiba la Ufaransa.

https://p.dw.com/p/1Hsoa
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent FabiusPicha: picture-alliance/dpa/E. Laurent

Maafisa wa serikali nchini Ufaransa wamethibitisha leo kwamba Waziri Fabius amejiuzulu wadhifa wake na kwa maana hiyo ameamua kujiondoa kwenye siasa za mstari wa mbele baada ya kuwamo katika medani hiyo kwa miaka zaidi ya 30.

Bwana Fabius alionekana akiwapungia watu wakati alipokuwa anatoka kuhuduhuruia kikao chake cha mwisho cha baraza la mawaziri leo asubuhi. Mwenyewe amethibitisha kwamba amejiuzulu wadhifa wake, hatua itakayosababisha kufanyika mabadiliko ya baraza la mawaziri baadae mnamo wiki hii.

Muda mfupi tu baada ya kujiuzulu ,Rais Francois Hollande alimteua kuwa Rais wa Baraza la Katiba, chombo kikuu cha mamlaka ya katiba nchini Ufaransa. Hata hivo msemaji wa serikali ameeleza kwamba bwana Fabius ataendelea kuwamo katika serikali, madhali bado hajapitia kwenye tume za kumthibitisha kuwa rais wa baraza hilo.

Baraza la mawaziri kubadilishwa

Kujiuzulu kwa bwana Fabius kutafuatiwa na mabadiliko ya baraza la mawaziri yatakayompa Rais Francois Hollande fursa ya kuijenga upya timu atakayoingia nayo katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwaka ujao nchini Ufaransa.

Waziri Fabius kwenye mkutano juu ya tabia nchi
Waziri Fabius kwenye mkutano juu ya tabia nchiPicha: Getty Images/AFP/F. Guillot

Bwana Fabius mwenye umri wa miaka 69 alikuwa Waziri Mkuu kijana kuliko wengine wote katika historia ya Ufaransa. Aliushika wadhifa huo wakati akiwa na umri wa miaka 37 mnamo mwaka wa 1984.

Katika wadhifa wa waziri wa mambo ya nje bwana Fabius alishiriki katika mazungumzo yaliyoleta makubaliano baina ya Iran na mataifa sita makubwa juu ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo. Miongoni mwa mafanikio yake pia ni kufikiwa mkataba wa kimataifa juu ya tabia nchi .

Bwana Fabius alikuwa mwenyekiti wa mazungumzo ya wiki mbili yaliyofanyika mjini Paris yaliyowezesha kufikiwa kwa mkataba huo. Licha ya kuitwa msoshalisti wa mvinyo, mara nyingine, Fabius ameweza kuthibitisha umahiri katika siasa za kimataifa.

Lakini siyo bila ya kuandamwa na kashfa. Baada ya majasusi wa Ufaransa kubainika, baada ya meli ya walinzi wa mazingira ,Rainbow Worrior kuzamishwa nchini New Zealand Fabius alikiri baadae kwamba meli hiyo ilizamishwa kwa kupigwa bomu na majasusi wa Ufaransa. Hapo awali serikali ya Ufaransa ilikanusha kuhusika na tukio hilo.

Meli hiyo ilikuwa njiani kuwapeleka wanaharakati waliokuwa wanakwenda kupinga kufanyika majaribio ya nyuklia.

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman