Waziri Fischer amezungumza na Viongozi wa Palestina
14 Julai 2005Ramallah:
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Joschka Fischer, leo anamaliza ziara yake ya siku mbili katika Mashariki ya Kati. Amezungumza na Rais Mahmud Abbas wa Palestina na Waziri Mkuu Ahmed Korei. Mazungumzo yao yamehusu mpango wa Waisraeli wa kuwahamisha Walowezi wa Kiyahudi katika yale maeneo ya Wapalestina. Zoezi litakaloanza Agosti 17 mwaka huu. Bw. Fischer, wakati wa mazungumzo yake na Waziri mwenzake wa Israeli, Silvan Shalom, mjini Jerusalem, amesema kuwa uamuzi huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mpango wa amani wa kimataifa na lengo la kuwa na nchi mbili zitakazoishi kwa amani. Waziri Fischer ameihakikishia Israeli kuwa Ujerumani iko tayari kusaidia na kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafakiwa. Bw. Fischer atarudi Ujerumani baadaye leo.