1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Heiko Maas afanya ziara ya kwanza Uturuki

5 Septemba 2018

Wakati Uturuki ikitafuta kuboresha uhusiano na washirika wake wa Ulaya, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas anafanya ziara yake ya kwanza nchini humo. Nchi hizo mbili zina hamu ya kuufufua uhusiano wao.

https://p.dw.com/p/34JVq
Berlin - PK Heiko Maas und Ditmir Bushati
Picha: picture-alliance/AA/A. Hosbas

Waziri Heiko Maas atakutana na mwenzake wa Uturuki Mevlüt Cavusoglu mjini Ankara wakati wa alasiri kwa ajili ya kufanya mazungumzo. Mkutano huo ndio unaashiria mwanzo wa ziara yake ya siku mbili nchini Uturuki. Ratiba imejaa na orodha ya matatizo ni ndefu kama vile, kuhusu raia wa Ujerumani wanaozuiliwa nchini Uturuki, marufuku kwa wabunge wa Ujerumani kwenda kwenye kambi ya jeshi la anga ya Incirlik, ambayo pia ilitumiwa na wanajeshi wa Ujerumani pamoja na maneno makali aliyotumia rais Erdogan mara kwa mara kumtuhumu kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwamba anatumia mbinu za mafashisti wa Nazi dhidi ya Waturuki wanaoishi Ujerumani na yote hayo ni ishara tosha kwamba uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki sio shwari.

Na bila shaka kwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, suala la kuachiwa kwa raia wa Ujerumani waliomo kwenye magereza ya Uturuki ni suala analolipa kipaumbele. Ikumbukwe bado kuna Wajerumani saba waliofungwa gerezani nchini Uturuki kwa sababu za kisiasa tangu kushindwa kwa jaribio la kutaka kuipindua serikali ya rais Erdogan mnamo mwaka 2016. Watatu kati ya wafungwa hao wana uraia wa nchi mbili - Ujerumani na Uturuki.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlüt Cavusoglu
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlüt CavusogluPicha: Getty Images/M. Gottschalk

Wakati ambapo Uturuki inatafuta kuuimarisha uhusiano wake na Ujerumani pamoja na bara la Ulaya kwa jumla bila shaka itaitumia ziara hiyo ya waziri Heiko Maas kujaribu kulainisha uhusiano wake na Ujerumani.  Wakati ambapo mivutano inaendelea kati ya Uturuki na Marekani pamoja na kudorora kwa uchumi wa Uturuki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas anafanya ziara nchini Uturuki katika wakati ambapo nchi hiyo inahitaji sana washirika wa kuaminika. Lakini hili halitawezekana kwani linahitaji hatua na maamuzi ya kisiasa kutoka kwa rais Recep Erdogan. Wakati huo huo ziara hiyo ya waziri Maas inatazamwa kama ni ya kuweka msingi kabla ya ziara ya rais Erdogan nchini Ujerumani anayotarajiwa kufanya mwisho wa mwezi huu.

Mtaalamu wa masuala ya Uturuki na mkurugenzi wa taasisi ya mafunzo ya kimataifa katika chuo kikuu cha Bremen Roy Karadag amesema anaamini kwamba Wajerumani waliofungwa nchini uturuki wataachiwa hivi karibuni ila sio bure. Amesema wafungwa hao wataweza tu kuwa huru lakini kwa kuzingatiwa maslahi ya Uturuki ya kiuchumi, kifedha na kuungwa mkono kisiasa.

Kushoto: Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Kulia Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kushoto: Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Kulia Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Pia mojawapo katika ajenda kwenye ziara ya waziri Maas ni kuhusu hali ya baadaye ya mgogoro wa nchini Syria. Serikali ya Syria inajiandaa kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya ngome kuu na ya mwisho ya waasi katika jimbo la Idlib ambapo Umoja wa Mataifa umeihibitisha kwamba huo ni mgogoro mpya wa kibinadamu. Uturuki, ambayo tayari imewachukua wakimbizi wa Syria karibu milioni 3.5 inaweza kukabiliwa na wimbi jingine la wakimbizi. Roy Karadag amesema jambo moja la uhakika ni kwamba nia ya Ujerumani ni kuzuia wakimbizi kuingia Ulaya. Na inafahamu kuwa Uturuki ni mshirika muhimu katika suala hilo la wakimbizi na kwa hilo Ujerumani inahitaji msaada wa Uturuki.

Mwandishi: Zainab Aziz/ DW Seda Serdar/Heinrich Daniel/p.dw.com/p/34J42

Mhariri:Josephat Charo