1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu Congo akubali kujiuzulu

Admin.WagnerD29 Januari 2021

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Sylvester Ilunga Ilunkamba amesalimu amri na kukubali kujiuzulu baada ya kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye.

https://p.dw.com/p/3oZ17
Sylvestre Ilunga Ilunkamba des. Premierminister DR Kongo
Picha: Presidence RDC

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Sylvester Ilunga Ilunkamba amesalimu amri na kukubali kujiuzulu ingawa amesema kuwa anasubiri kuarifiwa ili kutekeleza majukumu yake. Tangazo hilo kalitoa jana saa chache tu kabla ya kutimia muda wa saa 24 aliopewa na bunge la Kongo kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Félix Tshisekedi.

Baada ya kupigiwa kura na bunge ya kutokuwa na imani naye siku ya Jumatano, Ilunkamba alikuwa amekataa kujiuzulu akipinga uhalali wa ofisi ya kaimu spika kumualika na kumsikiliza waziri mkuu. 

Sylvester Ilunga Ilunkamba kasisitiza maoni yake kuhusu uhalali wa ofisi ya kaimu spika. Katika tangazo lake, amesema kwamba anaendelea kuiheshimu katiba na sheria ya nchi hii, na hivyo ametambua umahiri wa bunge kuchunguza hoja ya lawama dhidi ya serikali yake. Tangazo hilo lilisomwa na Albert Lieke Milayi ambaye ni msemaji wa Ilunga Ilunkamba.

''Kwa kuzingatia kuwa wabunge wanaounda bunge la kitaifa na ambao walichaguliwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2018 waliipigia kura Jumatano, hoja ya lawama dhidi ya serikali yangu, nasubiri taarifa ya uamuzi huu ili kutekeleza majukumu yangu kufuatana na katiba'', amesema Lieke Milayi.

Hatua hiyo ambayo ameichukuwa Sylvester Ilunga imepokelewa vizuri na mwanzilishi wa hoja hiyo iliyomuangusha waziri mkuu na serikali yake. Chérubin Okende, mbunge kutoka chama cha Ensemble Pour la République, cha Moses Katumbi amesema huo sasa ndiyo uthibitisho wa kukomaa kisiasa.

Alisema, ''nadhani baada ya kutambua uhuru wa bunge maalum ambalo lina uwezo wa kuchunguza hoja ya kukosoa, Profesa Ilunga Ilunkamba anainuka na hivyo anastahili kupewa sifa.''

Kwa upande wake PPRD, chama cha rais wa zamani wa Kongo Joseph Kabila wanaendelea kupinga kujiuzulu kwa waziri huyo mkuu. François Nzekuye ni mbunge wa chama cha PPRD.

''Lazima waachane na waziri mkuu hadi ofisi ya kudumu itakapoidhinishwa, halafu wataanzisha tena hoja dhidi yake ili tuone wakati huo, ikiwa waziri mkuu ataanguka. Sisi tunategemea uhalali.''

Upande wa bunge la taifa, mchakato unaendelea kuhusu uchaguzi wa ofisi ya kudumu unaotarajiwa kufanyika Jumatano ijayo.

Wahlen im Kongo
Rais wa zamani Joseph Kabila na chama chake wanaipinga hatua hiyo ya kujiuzulu kwa waziri mkuu Picha: picture-alliance/AP/J. Delay

Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.