1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Soo ajiuzulu baada ya upinzani kushinda uchaguzi wa bunge

11 Aprili 2024

Waziri Mkuu wa Korea Kusini na maafisa waandamizi wa ofisi ya rais wamewasilisha maombi ya kujiuzulu kwa wingi leo baada ya chama chao tawala kushindwa vibaya katika uchaguzi wa bunge

https://p.dw.com/p/4eer4
Han Duck-soo
Waziri Mkuu wa Korea Kusini Han Duck-sooPicha: Jung Yeon-je/AFP via Getty Images

Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa Rais mhafidhina Yoon Suk Yeol. Han Duck-soo na washauri wote waandamizi wa rais Yoon, isipokuwa tu wale wanaohusika na masuala ya usalama, wamewasilisha maombi ya kujiuzulu, kwa mujibu wa ofisi ya rais. Taarifa hiyo haijasema maramoja kama Rais Yoon aliwakubalia maombi hayo.

Mamlaka kamili nchini Korea Kusini yako katika wadhifa wa rais, lakini waziri mkuu ndiye afisa wa pili mwenye nguvu na huiongoza nchi ikiwa rais atakuwa hana uwezo kutokana na hali fulani.

Upinzani washinda uchaguzi wa bunge nchini Korea Kusini

Matokeo ya uchaguzi huo wa jana yana maaana vyama vya upinzani vya kiliberali vitaendeleza udhibiti wao wa bunge hadi pale Yoon atakapokamilisha muhula wake wa miaka mitano katika mwaka wa 2027.

Takwimu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi zinaonyesha chama cha Democratic Party DP na chama chake tanzi kinatarajiwa kunyakua zaidi ya viti 175 kati ya 300 katika bunge jipya, baada ya zaidi ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa. Chama kingine cha kiliberali kinachozingatiwa kuwa mshirika wa DP kinatarajiwa kushinda angalau viti 12. 

Wataalamu wanasema hali hiyo inaweza kuathiri utekelezaji wa sera zake za ndani na kudhoofisha udhibiti wake wa chama tawala huku akikabiliwa na changamoto kubwa ya kisiasa kutoka kwa upinzani wakati wa miaka yake mitatu inayobaki katika utawala wake.