Hotuba ya Waziri Mkuu May yasubiriwa kwa hamu
17 Januari 2017Katika hotuba inayosubiriwa kwa hamu, huenda Waziri mkuu May akaashiria kwamba Uingereza inaelekea katika kile ambacho wachambuzi wanakiita kuwa”hali ngumu ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Bibi May atatoa hotuba yake kwenye jingo la Lancaster katikati mwa jiji la London, mahala ambapo ni kitovu cha shughuli za kidiplomasia na matangazo muhimu.
Kwa mujibu wa yaliomo ndani ya Hotuba hiyo iliotawanywa mapema kwa vyombo vya habari na makao makuu ya Waziri mkuu ya nambari kumi mtaa wa Downing, Bibi May anatarajiwa kueleza wazi kwamba , " hakuna kujitoa nusu , huku akisisitiza kwamba kujitoa yaani "Brexit " kunamaanisha kujitoa.
Hapana shaka muelekeo wake utashangiriwa na waingereza wanaotaka nchi yao ijitowe kutoka Umoja wa Ulaya na kuwavunja moyo mno wanaotaka ibakie kuwa mwanachama, ambao wanaofu kwamba kujiondoa kutrakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Uingereza.
Hotuba yake itagusia kila pembe ya mkakati wake wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya wa wanachama 28 , baada ya miezi kadhaa ya taharuki na vuta nikuvute. Wadadisi walikwisha ashiria hivi karibuni kwamba Uingereza itataka kujitoa kikamilifu, ili iweze kuwa na malaka ya kushughulikia kikamilifu suala la wahamiaji.
Hotuba ya Waziri mkuu May imetawala hii leo katika magazeti ya Uingereza, huku Daily Mail linalounga mkono kujitoa, likionekana kusherehekea. Kichwa cha maneno cha toleo lake kinasema,” Uingereza huru na mpya ya Theresa May.” Hata hivyo gazeti la Guardian linalopendelea Uingereza ibakie kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, limewaonya wanaopinga likisema watajuta.
Sarafu ya Uingereza”Sterling” imeimarika kidogo leo baada ya kuteremka thamani Jumatatu katika hali kiwango kisichowahi kushuhudiwa kwa miaka 31 iliopita. Pamoja na hayo waziri wa fedha Philip Hammond alisema anataka Uingereza iendelee kutambuliwa kuwa ina uchumi utakaofuata utaratibu wa Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na utaratibu wakodi na viwango sawa na Umoja huo. Bibi May ameahidi kuanza rasmi mazungumzo na Umoja wa Ulaya mwezi Machi na Mkuu wa Umoja huo anayehusika na mazungumzo hayo Michel Barnier amesema makubaliano yanapaswa kufikiwa kabla ya uchaguzi wa bunge la Ulaya 2019.
Uingereza itakayojitoa kwenye Umoja huo, ni jambo lililopewa msukumo Jumapili na Rais mteule wa Marekani Donald Trump ambaye alisema anaunga mkono kuwepo kwa mkataba wa haraka wa kibiashara kati ya Marekani na Uingereza. Lakini hata ikiwa mpango wa Waziri mkuu wa Uingereza hii leo utapata uungaji mkono mkubwa nchini mwake, bado kuna changamoto za kisheria ambazo zinaweza kuucheklewesha mpango wa kujitoa.
Mahakama kuu ya Uingereza inatarajiwa kuamua baadae mwezi huu, iwapo Bibi May kwanza atahitaji kibali cha bunge kabla ya kuanza mazungumzo ya kujitoa katika Umoja wa ulaya , jambo ambalo huenda likachelewesha mazungumzo .
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman / afp
Mhariri: Josephat Charo