Waziri Mkuu Truss ahaha kurejesha imani ya chama chake
5 Oktoba 2022Baada ya muda wa chini ya mwezi mmoja madarakani hatua ya waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss ya kughairi kuwapunguzia kodi watu wenye vipato vya juu imemfanya waziri mkuu huyo aingie katika lawama, siyo kwamba alipata ushauri mbaya bali pia alinadiwa vibaya kuwa mwanamke anayesimamia kauli zake.
Waziri Mkuu Truss aligeuza uamuzi muda wa saa 24 baada ya kutetea sera yake ya kupunguza kodi. Wabunge wake walimtanabahisha kwamba alikuwa anajiingiza kwenye hatari ya kushindwa uchaguzi kwa kufufua hisia kwamba chama cha wahafidhina hakiwajali maskini.
Soma pia: Sarafu ya Uingereza yaanguka dhidi ya dola
Kwenye mkutano wa mwaka wa chama hicho unaofanyika mjini Birmingham, baadhi ya wabunge walisema waziri mkuu Truss na waziri wake wa fedha Kwasi Kwarteng waliwasikiliza wale wasiowajali masikini.
Sasa waziri mkuu huyo anacho kibarua cha kurejesha imani na kuzikabili changamoto za kisera kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2024 nchini Uingereza.
Wakati huo huo Liz Truss amekataa kusema iwapo posho kwa wananchi zinapandishwa kwenda sambamba na mfumuko wa bei. Hata hivyo ameeleza kuwa serikali yake itatekeleza sera ya fedha ya kuwajibika.
Soma pia: Mfahamu Liz Truss na safari yake kisiasa
Baadhi ya wabunge wa chama cha wahafidhina wanakumbusha aliyosema waziri mkuu wa zamani Theresa May, mnamo mwaka 2002 kwamba chama cha Conservative hakiwajali masikini na jumuiya za wachache.
Chama cha Labour chanufaika na makosa ya Truss
Kura za maoni zinaashiria uwezekano wa chama hicho kuangushwa na chama cha wapinzani cha Labour katika uchaguzi ujao. Baadhi ya wabunge wa chama hicho cha wahafidhina wanasema wazi kwamba waziri mkuu Truss na mawaziri wake wanapaswa kubeba lawama. Wengine wamesema mawaziri wapya hawajui wanalolifanya .
SOma pia: Liz Truss waziri mkuu mpya Uingereza
Ni muda mrefu uliopita tangu waziri mkuu Truss alipokuwa anamwagiwa sifa kuwa kiongozi aliyefaa kukiongoza chama cha wahafidhina baada ya waziri mkuu wa hapo awali Boris Johnson kutimuliwa na waasi wa ndani ya chama hicho.
Waziri Mkuu Liz Truss alisema, hatatoa ahadi ambazo hawezi kuzitimiza. Alisema kuwa yeye ni mkweli na kwamba wakati wote anasema kulingana na mambo yalivyo.
Soma pia: Truss afanya kikao chake cha kwanza na timu yake ya mawaziri
Baada ya kuteuliwa mnamo tarehe 6 mwezi Septemba, aliwaongoza waingereza katika maziko ya Malkia Elizabeth wa pili, lakini baada ya kurejea kwenye shughuli za siasa alitaka kuchukua hatua za haraka! Alitaka kuanza kwa kupunguza kodi.
Mbunge Marco Longhi, amesema hatua hiyo haikubaliki. Watu wa eneo lake la bunge wamempinga waziri mkuu Truss juu ya sera hiyo. Hata baadhi ya wafuasi wa bibi Truss kwenye mkutano wa mjini Birmingham walishangazwa na kasi ya mwanasiasa huyo na wamemtaka apunguze kasi hiyo.
Hata hivyo baadhi ya wabunge wamempongeza waziri wa fedha Kwasi Kwarteng kwa kubadilisha msimamo. Wamesema huu ni wakati wa kusimama pamoja katika chama. Wabunge wa chama cha wahafidhina sasa wanaunga mkono sera itakayoleta ustawi wa uchumi.
Chanzo: RTRE