Waziri Mkuu wa Haiti atafuta msaada zaidi dhidi ya magenge
6 Oktoba 2024Waziri mkuu wa Haiti Garry Conille mnamo Jumamosi alianza ziara katika Umoja wa Falme za Kiarabu na Kenya kwa lengo la kutafuta usaidizi wa kiusalama.
Ziara hii inajiri baada ya genge la Gran Grif kuvamia eneo la Artibonite magharibi mapema Alhamisi, na kuua watu wasiopungua 70, wakiwemo watoto wachanga, na kuwalazimu wakazi zaidi ya 6,000 kuyakimbia makaazi yao.
Mauaji hayo yalisababisha mshtuko mkubwa licha ya kwamba taifa hilo limezoea kuzuka kwa vurugu, wakati jeshi la polisi la taifa limezidiwa na matukio ya uhalifu.
Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mwaka mwengine kwa kikosi cha usalama cha kimataifa ambacho kimekusudiwa kusaidia polisi wa eneo hilo kurudisha amani na utulivu katika taifa hilo la Karibia.