Waziri Mkuu wa Lebanon Hariri akubali mwaliko wa Ufaransa
16 Novemba 2017Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bonn ambako alikuwa akihudhuria mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi, rais wa Ufaransa Emanuel Macron alisema Hariri pamoja na familia yake wamealikwa kwa ajili ya kukaa nchini Ufaransa kwa siku chache tu lakini akasema alikuwa hampatii kiongozi huyo hifadhi ya kisiasa.
Macron amesema kuna haja ya kuwa na viongozi ambao wako huru katika kutoa maoni yao na kuongeza kuwa ni muhimu kwa Hariri kuweza kuendeleza mchakato wa kisiasa nchini mwake katika siku na wiki zijazo.
Tangazo hilo linakuja mnamo wakati waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean- Yves Le Drian akiwa nchini Saudi Arabia ambako anakutanha na Hariri pamoja na mfalme wa Saudia.
Hariri akitolea mfano wa Iran na kundi la Hezbollah kuingilia masuala ya ukanda huo alitangaza kujiuzulu wadhifa wake akiwa nchini Saudi Arabia na tangu wakati huo hajarejea nchini Lebanon na Rais wa Lebanon bado hajakubali kujiuzulu kwake.
Rais wa Ufaransa Emanuel Macron hapo jana Jumatano alimualika Hariri na familia yake nchini Ufaransa huku kukiwa na madai kuwa Saudi Arabia inamshikilia kiongozi huyo kama mfungwa.
Kwa upande mwingine ofisi ya rais wa Ufaransa imesema baada ya kuzungumza na mwana wa mfalme Mohammed bin Salman na waziri mkuu wa Lebanon Saad al Hariri rais Macron ameamua kumualika mwanasiasa huyo pamoja na familia yake.
Hariri pasipo kutarajiwa alitangaza kujiuzulu wadhifa wake kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa kupitia Televisheni nchini Saudi Arabia Novemba 4 na siku 11 zilizofuatia kumekuwepo na uvumi kuhusiana na hali ya waziri mkuu huyo wa Lebanon.
Hapo jana Jumatano rais wa Lebanon Michel Aoun alisema Hariri alikuwa akizuiliwa na maafisa wa Saudi Arabia na kutaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati. Aoun alikataa kukubali kujiuzulu kwa Hariri na kumtaka arejee Beirut.
Hayo yanajiri huku Saudi Arabia ikikanusha kuwa Hariri alikuwa akishikiliwa.
Rais wa Ufaransa Emanuel Macron tayari alikwishafanya ziara ya kushitukiza nchini Saudi Arabia Alhamisi iliyopita na kukutana na mwana wa mfalme Mohammed bin Salman mnamo wakati mivutano ikiibuka kati ya Saudi Arabia na Iran.
Mwandishi: Isaac Gamba/dw/ape
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman