1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan aondolewa madarakani

Zainab Aziz Mhariri: Lilian Mtono
10 Aprili 2022

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ameondolewa mamlakani baada ya bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.

https://p.dw.com/p/49iat
Pakistan Premierminister Imran Khan
Picha: Anjum Naveed/AP/picture alliance

Washirika wake kadhaa na chama kikuu kwenye muungano na chama chake hawakumuunga mkono kwenye kura hiyo huku wakimlaumu kwa kusabisha kuanguka kwa uchumi wa Pakistan na kushindwa kutekeleza ahadi alizozitoa kwenye kampeni.

Wanajeshi nje ya Bunge la Pakistan.
Wanajeshi nje ya Bunge la Pakistan.Picha: Anjum Naveed/AP Photo/picture alliance

Khan awali alijaribu kuzuia kura hiyo kwa kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema lakini Mahakama ya juu nchini Pakistan iliamuru kura hiyo iendelee. Upinzani ulishinda baada ya wabunge wapatao 174 kupiga kura ya kutokuwa na Imani na Imran Khan. Bunge la Pakistan lina jumla ya viti 342

Soma:Waziri Mkuu wa Pakistan akabiliwa na kura ngumu ya kutokuwa na imani naye

Spika wa bunge, Ayaz Sadiq alitangaza matokeo mapema leo Jumapili baada ya kumalizika zoezi hilo la kupiga kura lililochukua takriban saa 13. Wabunge wachache tu wa vyama vilivyo katika muungano na chama cha Imran Khan cha Tehreek-i-Insaf au Vuguvugu la Pakistan la Haki waliohudhuria kikao hicho, yeye mwenyewe hakuhudhuria.

Waziri Mkuu wa Pakistan aliyeondolewa madarakani Imran Khan.
Waziri Mkuu wa Pakistan aliyeondolewa madarakani Imran Khan.Picha: Akhtar Soomro/File Photo/REUTERS

Waziri Mkuu Imran Khan mwenye umri wa miaka 67 ameondolewa baada ya kuiongoza Pakistan kwa miaka mitatu na nusu. Taifa hilo linalomiliki silaha za nyuklia lina idadi ya raia milioni 220. Jeshi limetawala nchini humo kwa karibu miaka 75, nusu ya historia ya nchi hiyo. 

Bunge linatarajiwa kukutana Jumatatu kumchagua waziri mkuu mpya. Shehbaz Sharif anayepigiwa upatu wa kupokea kijiti hicho cha uwaziri mkuu amesema hatua hiyo inafungua fursa ya mwanzo mpya. Anasifiwa kuwa ni msimamizi mzuri. Sharif, mwenye umri wa miaka 70, ni mdogo wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif aliyeshikilia wadhfa huo mara tatu.

Katikati: Shehbaz Sharif kiongozi wa upinzani anayetarajiwa kuchukua nafasi ya Waziri Mkuu wa Pakistan.
Katikati: Shehbaz Sharif kiongozi wa upinzani anayetarajiwa kuchukua nafasi ya Waziri Mkuu wa Pakistan.Picha: Tanvir Shahzad/DW

Zoezi la kupiga kura lilicheleweshwa kkutokana na kuahirishwa kwa mara kadhaa na hotuba ndefu za wabunge wa chama wa chama cha Khan, ambao waliilaumu Marekani kwa kuunga mkono njama ya kumwondoa Imran Khan nyota wa mchezo wa kriketi aliyegeuka mwanasiasa.

Awali Khan aliilaumu Marekani kwa kuunga mkono hatua hizo za kumwondoa madarakani kwa sababu alikuwa ameitembelea Urusi na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin mara tu baada ya Urusi kuivamia Ukraine mnamo Februari 24.  Marekani imekanusha madai hayo.

Soma:Wabunge Pakistan kuanza kupiga kura ya kutokuwa na imani na Khan

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan aliyeondolewa madarakani alikuwa anaipinga Marekani katika kipindi chake chote, na atakumbukwa kwa kuunga mkono hatua yaTaliban ya kuirejesha Afghanistan mikononi mwake mwaka jana ambapo aliitaka jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Taliban.

Muhammad Ali Khan, mbunge kutoka kwenye chama cha Imran Khan cha Tehreek-i-Insaf, amesema Waziri Mkuu huyo alipambana hadi mwisho na bila shaka atarejea uongozini hapo baadaye.

Vyanzo:RTRE/AP