1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Pakistan kukutana na kundi la Taliban

Sylvia Mwehozi
24 Julai 2019

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na kundi la wanamgambo la Taliban mara atakaporejea nchini mwake, kama sehemu ya juhudi za kukomesha vita vya miaka 18 nchini Afghanistan. 

https://p.dw.com/p/3MfpN
US-Präsident Donald J. Trump empfängt den pakistanischen Ministerpräsidenten Imran Khan
Picha: picture-alliance

Khan ameyasema hayo mjini Washington wakati wa ziara yake rasmi ya kwanza nchini Marekani, ambako alikutana na mwenyeji wake Rais Donald Trump. Khanalisema pia alizungumza na Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani na wakakubaliana kwamba akirejea atafanya juhudi za kukutana na kundi la Taliban ili waweze kuketi katika meza ya mazungumzo na serikali.

Alisema kundi hilo liliwahi kumtafuta miezi michache iliyopita baada ya kushinda uchaguzi wa Julai 2018, lakini hakuweza kukutana nalo kwa sababu serikali ya Kabul haikutaka na kwa kuwa alishikilia msimamo wake kwamba hakuna suluhisho ya kijeshi katika vita ya Afghanistan.

Khan ameongeza kwamba amekuwa na mazungumzo mazuri na Trump akisisitiza kwamba sasa Pakistan na Marekani ziko kwenye ukurasa mmoja kuhusiana na juhudi hizo. Marekani imekuwa ikijihusisha na kundi la Taliban lakini hadi sasa wamekataa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya Afghanistan, inayoichukulia kuwa ya kinafiki. Waafghanistan wana wasiwasi juu ya ushiriki wa Pakistan katika mustakabali wa nchi yao, lakini Khan anaamini kundi la Taliban linapaswa kushiriki uchaguzi mkuu ujao wa rais wa mwezi Septemba.

US-Präsident Donald J. Trump empfängt den pakistanischen Ministerpräsidenten Imran Khan
Imran Khan na rais Donald Trump katika Ikulu ya White HousePicha: picture-alliance

Pamoja na juhudi hizo za mazungumzo ya amani, Afghanistan walishangazwa na kauli iliyotolewa wiki hii na Trump kwamba anaweza kuruhusu jeshi kuiangamiza Afghanistan na kuiondoa katika "uso wa dunia" ndani ya wiki moja tu. Kauli hiyo ya Trump ilitoa wasiwasi kwa sababu vita haijakuwa baina ya Afghanistan na Marekani. Kwa miaka 10 vikosi vya Afghanistan vimepigana kando ya washirika wake wa Marekani na Jumuiya ya kujihami NATO dhidi ya Taliban.

Kwa miaka kadhaa pia Afghanistan inaituhumu Pakistan kwa kuchochea vita katika nchi yao kwa kuwahifadhi wanamgambo na hivyo kufanya mashambulizi kwa urahisi. Marekani yenyewe pia imekuwa ikiituhumu Pakistan kwa kuwafadhili wanamgambo na kudai inafanya vigumu kuliangamiza kundi hilo, ambalo hivi sasa linadhibiti karibu nusu ya Afghanistan lakini sio mijini.

Uhusiano huo yataanzisha ukurasa mpya wa Khan na Trump ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Paksitan. Utawala wa Obama uliongeza idadi ya misaada ya kijeshi na kiuchumi hadi kufikia dola bilioni 3 kwa mwaka, lakini Trump alizipunguza hadi dola milioni 70 katika kipindi cha mwaka huu wa fedha.

Vyanzo: AP/AFP