1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Sudan kurejea madarakani?

3 Novemba 2021

Jeshi nchini Sudan bado linaendelea na majadiliano na waziri mkuu aliyeondolewa madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi wiki iliyopita, Abdalla Hamdok.

https://p.dw.com/p/42VyN
Sudan Abdullah Hamduk Putsch Protest Ausschreitungen
Picha: picture alliance/dpa/XinHua

Kulingana na duru zilizoko karibu kabisa na waziri mkuu huyo mazungumzo yanayoendelea sasa yanaangazia uwezekano wa kiongozi huyo kurejea kuiongoza serikali. 

Soma Zaidi: Mamia wapinga kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Sudan

Kumekuwepo na taarifa zinazokinzana mapema leo kuhusiana na mazungumzo hayo baada ya kituo cha televisheni kinachomilikiwa na Saudi Arabia cha al-Arabiya kuripoti kwamba waziri mkuu Abdalla Hamdok aliyepinduliwa kupitia mapinduzi ya kijeshi amekubali kurejea kuiongoza serikali ingawa hakikuweka wazi vyanzo vya taarifa hiyo.

Katika ripoti nyingine kituo cha televisheni cha al Hadath chenye mahusiano na al Arabiya kiliripoti kikinukuu baadhi ya vyanzo vilivyokutana na waziri mkuu huyo wiki iliyopita kwamba anataka wafungwa wa kisiasa waachiwe huru kama moja ya masharti ya kukubali kuingia kwenye mazungumzo ya kina ya kuongoza tena serikali. 

Hata hivyo muda mfupi baadae chanzo kilichopo karibu kabisa na waziri mkuu huyo kilikana taarifa hiyo kikisema hakukuwa na makubaliano yoyote yaliyofikiwa kati ya Hamdok na viongozi wa kijeshi na mazungumzo bado yanaendelea.

Sudan General Abdel Fattah al-Burhan
Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan anadai kwamba mapinduzi hayo yaliepusha vita vya raia. Picha: Sudan TV/AFP

Juhudi za kusaka suluhu ya mzozo huo zimekuwa zikiendelea kwa siku kadhaa na kulingana na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, pande zote zinataka kujinasua kwenye mzozo huo wa kisiasa.

Hamdok amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu serikali yake ilipoangushwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na jenerali mwandamizi nchini humo Abdel Fattah al-Burhan. Mapinduzi hayo pamoja na mambo mengine yamezorotesha mchakato wa mabadilishano ya madaraka lakini pia kuyafanya mataifa ya magharibi na wafadhili kusitisha misaada.

Hapo jana mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Marekani alimtolea mwito Jenerali Burhan kuirejesha nchi kwenye utawala wa kiraia wakati kiongozi huyo wa kijeshi akizidi kuelemewa na shinikizo la kusuluhisha mzozo baina ya jeshi na raia.

Mjumbe huyo maalumu wa Marekani kwenye Upembe wa afrika Jeffrey Feltman alisema Jenerali Burhan anatakiwa kumruhusu waziri mkuu Hamdok na baraza lake kurejea kwenye majukumu yao na kuwaachia maafisa wa serikali na wanasiasa wanaoshikiliwa kufuatia mapinduzi hayo.

Burhan mwenyewe alisema kwamba mapinduzi hayo yalikuwa ni muhimu ili kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe akiangazia kile alichodai ni kuongezeka kwa mgawanyiko miongoni mwa makundi ya kisiasa. Hata hivyo mapinduzi hayo yalifanyika chini ya mwezi mmoja kabla ya utawala wa kijeshi kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.

Tizama Zaidi: 

Maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi Sudan yaendelea

Mashirika: RTRE/APE