1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Uingereza afanya ziara barani Afrika

28 Agosti 2018

Bibi Theresa May ametangaza mipango ya kuongeza vitega uchumi barani Afrika baada ya nchi yake kujiondoa Umoja wa Ulaya. Ametoa ahadi hiyo nchini Afrika Kusini, ambayo ni kituo cha kwanza cha ziara yake ya barani Afrika.

https://p.dw.com/p/33tvO
Theresa May in Südafrika
Picha: Reuters/M. Hutchings

Akihutubia kwenye bunge la Afrika Kusini mjini Cape Town Waziri Mkuu May aliahidi dola bilioni 5.1 kusaidia uchumi wa nchi za Afrika ili nchi hizo ziweze kutenga nafasi za ajira kwa ajili ya vijana, bibi May pia ameahidi kuleta mabadiliko ya kimsingi katika utaratibu wa kutoa misaada utakaozingatia changamoto za kiuchumi na kiusalama za muda mrefu kwa lengo la kupunguza umasikini barani Afrika.

Bibi May amesema, katika ziara yake barani Afrika anatarajia kujadili namna Uingereza itakavyoendeleza na kuimarisha ushirikiano huo pamoja na Afrika ili kuongeza vitega uchumi na hivyo kudumisha utulivu na usalama.

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/I. Forsyth

Theresa May ametumia fursa ya ziara yake nchini Afrika Kusini kutangaza mkataba wa kwanza wa serikali yake baada ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya. Lakini wakati huo huo amehakikisha kwamba Uingereza inadhamiria kuendeleza ushirikiano uliopo sasa baina ya Umoja wa Ulaya na nchi sita za kusini mwa Afrika, na amesema ushirikiano wa kweli siyo ule ambapo upande mmoja tu kuufanyia upande mwingine, bali ni pale nchi, wafanyabiashara na watu binafsi wanapofanya kazi kwa pamoja katika namna ya kuwajibika ili kufikia malengo ya pamoja.

Waziri Mkuu May amesema, miongoni mwa nchi tajiri duniani za kundi la  G7, anataka Uingereza iwe ya kwanza katika uwekeezaji vitega uchumi barani Afrika, hadi utakapofika mwaka 2022. Katika lengo hilo kampuni binafsi za Uingereza ndizo zitakazotoa mchango mkubwa wa kuziwezesha nchi za Afrika kustawisha uchumi kwa viwango vya matrilioni.

Rais wa Afrika wa kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika wa kusini Cyril RamaphosaPicha: Getty Images/AFP/R. Bosch

Waziri mkuu May amekabidhi rais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa kengele ya meli iliyokuwa inawasafirisha askari 600 wa Afrika Kusini walioangamia baada ya meli hiyo kuzama wakati wa vita vikuu vya kwanza mnamo mwaka 1917.

Rais Ramaphosa amesema kukabidhiwa kengele ya meli hiyo SS Mendi ni heshima kubwa kwa Afrika Kusini. Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May pia atafanya ziara nchini Kenya na Nigeria. 

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman