Waziri Mkuu wa Uingereza atetea jukumu lake katika vita vya Irak 2003
5 Machi 2010Waziri mkuu wa Uingereza anasema hakuzuia utoaji fedha kwa wanajeshi waliokwenda Iraq, lakini alikuwa hahusiki kwa karibu katika utoaji maamuzi ya kisiasa juu ya vita hivyo vya Iraq. Badala yake alikuwa akiarifiwa kikamilifu na alifanya kila alichotakiwa kufanya katika wadhifa wake kama waziri wa fedha, chini ya utawala wa Tony Blair. Ameutetea uamuzi wa kuingia vitani nchini Iraq, akisema kwamba Saddam Hussein alikuwa mtu aliyekiuka mara zote sheria ya kimataifa.
''Nafikiri ulikuwa ni uamuzi mgumu sana kuliko wakati mwingine wote, kuamua kwenda vitani. Naamini tulichukua uamuzi mzuri kutokana na sababu za kueleweka, kwa sababu kwa kipindi cha miaka kadhaa jumuiya ya kimataifa imekuwa ikimuomba Saddam Hussein azingatie sheria ya kimataifa na masharti ambayo aliyaafiki''
Gordon Brown Kufika mbele ya jopo la majaji linalochunguza juu ya vipi Uingereza ilivyohusika katika vita vya Iraq, ni hatua inayoonekana kama ni karata ya bahati nasibu, kisiasa, wiki chache kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika May 6. Vita vya Iraq vilivyosababisha wanajeshi 179 wa Uingereza kuuwawa ni suala ambalo limesalia kuwa muhimu kuelekea uamuzi wa wapiga kura nchini Uingereza. Wengi nchini humo wanamlaumu Tony Blair aliyekuwa waziri mkuu wakati huo kwa kuiingiza Uingereza katika vita vya Iraq. Hata hivyo, Gordon Brown amekiri kwamba maisha ya wengi yamekatishwa kupitia vita hivyo na kosa lilifanyika, lakini ni uamuzi mgumu uliostahili kuchukuliwa.
Otone
''Nafikiri tulikuwa hatuna njia nyingine ila kuingilia kati hali ya mambo ambapo kulikuwa na vitisho mara mbili vya kusababisha dunia kuingia katika vita vingine baada ya vita baridi. Kwanza ,kama nilivyogusia, ni hatua ya mataifa yasiyounga mkono ugaidi, na pili ni hatua iliyozihusisha nchi za kihalifu au katika suala la Iraq naweza kusema ilikuwa ni nchi ya maguvu. Na ikiwa ulimwengu unakubali kwamba unataka kuwa katika hali ya utulivu, basi, bila shaka, tunabidi kujiandaa kuchukua hatua za kimataifa. Ni kweli kwamba ni bora zaidi ikiwa nchi zote zitakubaliana katika kuchukua hatua ambayo ni lazima ichukuliwe, lakini kulikuwa na umuhimu wa kuchukua hatua mahala ambapo aidha kupitia ugaidi tungeiweka nchi yetu wenyewe hatarini au kupitia mataifa ya maguvu kwenye eneo hilo, na hapa nazungumzia Iraq, kuyatumbukiza maeneo yote ya nchi hiyo katika kitisho vilevile.''
Gordon Brown amekosolewa na maafisa wa ngazi ya juu serikalini pamoja na wakuu wa kijeshi kwa kushindwa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuwahami wanajeshi wa Uingereza.
Mwandishi Saumu Mwasimba/RTRE
Mhariri Othman Miraji.