1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brown kukutana na Obama leo.

Abdu Said Mtullya3 Machi 2009

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown yupo Marekani kwa ziara ya siku tatu.

https://p.dw.com/p/H4sl
Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, leo anatarajiwa kufanya mazungumzo na rais Barack Obama  wa Marekani ,na kuwa kiongozi wa kwanza wa Ulaya kukutana na rais huyo kwenye Ikulu mjini Washington.

Viongozi hao wanatazamiwa kujadili mgogoro wa uchumi ulioikumba dunia, mkakati mpya  juu ya Afghanistan na matayarisho ya  mkutano wa nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi- G 20 utakaofanyika mjini London.

Waziri mkuu wa Uingereza  Brown na rais  Barack Obama wa Marekani pia watazungumzia juu ya mkutano  wa viongozi wa nchi za jumuiya ya Nato utakaofanyika mjini Brussels.

Bwana Brown anaesema kuwa anataka mkakati mpya juu ya kuufufua uchumi wa   dunia,  anatafuta mshikamano wa Marekani katika juhudi za kufikia lengo hilo.

Uingereza na Marekani zimeshapitisha mipango kamambe juu ya kufufua uchumi tokea kusambaratika kwa mabenki kadhaa  makubwa ya nchi hizo.

Waziri mkuu Brown amesema anakusudia  kutumia fursa ya mazungumzo yake na rais Obama kutayarisha mkutano wa nchi tajiri na zinazoendelea  za G-20 utakaofanyika mjini London mwezi aprili utakaojadili mpango  mpya juu ya kufufua uchumi.

Hatahivyo,waziri mkuu Brown pia anatarajiwa  kusisitiza umuhimu wa kuepusha sera  za kujenga vizingiti vya kiuchumi na kibiashara katika uhusiano wa kimataifa.

Katika ziara yake nchini Marekani, bwana Brown pia atalihutubia bunge la nchi hiyo na  kuwa waziri mkuu wa  tano wa Uingereza kufanya hivyo .