Brown na Obama wakutana.
4 Machi 2009Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown anaendelea na ziara ya nchini Marekani amekutana na rais Barack Obama mjini Washington leo anatarajiwa kulihutubia bunge la nchi hiyo.
Waziri Mkuu Brown na mwenyeji wake rais Obama wamejadili haja ya kuratibisha juhudi zao katika kukabiliana na mgogoro wa uchumi ulioikumba dunia.
Waziri mkuu Brown ametoa mwito juu ya kuwapo mpango mpya wa kimataifa kama ule uliotekelezwa na Marekani katika kukabiliana na msambaratiko wa uchumi ulioikumba dunia mnamo miaka 1930.
Amesema katika miezi ijayo patakuwa na uwezekano wa kuanzisha mpango huo mpya wa kuzijumuisha nchi zote, kwa lengo la kurekebisha mfumo wa mabenki duniani.
Bwana Brown ambae ni kiongozi wa kwanza wa Ulaya kukutana na rais Obama kwenye Ikulu ya Marekani anatumai kuungwa mkono na Marekani katika dhamira ya kuanzisha udhibiti mkali katika mfumo wa mabenki wa kimataifa.
Kwenye mazungumzo yao viongozi hao wa Uingereza na Marekani pia walijadili mkutano wa nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi za G- 20 utakaofanyika mjini London mwezi ujao.Viongozi hao pia wamejadili hali ya Afghanistan inayozidi kuzorota.
Waziri Mkuu Brown leo anatarajiwa kuyahutubia mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani ambapo anatazamiwa kutoa mwito juu ya kusaidia katika juhudi za kuondoa vurumai iliopo katika mfumo wa mabenki.
Bwana Brown pia atatoa mwito juu ya kupinga sera za kujenga vizingiti katika uhusiano wa biashara na uchumi.