Waziri Mkuu Rishi Sunak aendeleza ukaidi mpango wa Rwanda
16 Novemba 2023Akizungumza baada ya hukumu hiyo kali iliyotikisa serikali yake, Waziri Mkuu Rishi Sunak ambaye aliahidi kuzuwia wahamiaji wanaowasili Uingereza katika boti ndogo ndogo kupitia ujia wa bahari wa English Channel, alisema hukumu hiyo haikuwa matokeo aliyoyataka huku akiapa kuendelea na mpango wake wa safari za kwanza za ndege za wahamiaji kwenda Rwanda msimu ujao wa machipuko.
Alisema mahakama ilithibitisha kuwa kanuni ya kuwahamisha waomba hifadhi katika nchi nyingine iliyo salama ni halali, licha ya kuhitimisha kwamba Rwanda haiko salama. Waziri Mkuu Sunak ameahidi kupitisha sheria bungeni, itakayohakikisha kuwa Rwanda itakuwa salama, na kuhakikisha mpango wake hauzuwiliwi na mahakama za kigeni.
Soma pia: Mahakama Uingereza yabatilisha kupeleka wakimbizi Rwanda
"Sikubaliani na uamuzi huu, lakini ninauheshimu na kuuafiki. Pia ninatangaza leo kwamba tutachukua hatua isiyo ya kawaida ya kuanzisha sheria ya dharura. Hii itawezesha Bunge kuthibitisha kwamba kwa mkataba wetu mpya, Rwanda iko salama," alisema Waziri Mkuu Sunak.
"Itahakikisha kwamba watu hawawezi kuchelewesha safari za ndege kwa kuleta pingamizi za kimfumo katika mahakama zetu za ndani na kukomesha sera yetu kuzuiwa mara kwa mara. Sitaruhusu mahakama ya kigeni kuzuia safari hizi za ndege," alisisitiza.
Uingereza na Rwanda zilisaini mkataba mwezi Aprili 2022 wa kuwapeleka wahamiaji wanaofika Uingereza kwa kudandia vyombo vya usafiri au kwa boti, katika nchi ya Rwanda, ambako maombi yao ya hifadhi yatashughulikiwa na endapo watafanikiwa, wangesalia huko.
Serikali ya Uingereza inahoji kuwa sera hiyo itawazuia watu kuhatarisha maisha yao kwa kuvuka mojawapo ya njia za meli zenye shughuli nyingi zaidi duniani, na itavunja mtindo wa biashara wa magenge yanayosafirisha watu kimagendo.
'Aibu ya kihistoria' na kinyume cha maadili ya Uingereza
Mpaka sasa hakuna mtu aliyehamishiwa Rwanda baada ya mpango huo kupingwa mahakamani. Wanasiasa wa upinzani, mashirika ya wakimbizi na mashirika ya haki za binadamu yanasema mpango huo umekosa maadili na hautekelezeki.
Soma pia: Mpango wa UK kuwapeleka wahamiaji Rwanda waenda mahakamani
Shirika la hisani la ActionAid UK limeitaja hukumu ya mahakama ya juu kuwa uthibitisho wa maadili ya Uingereza ya huruma na utu. Nalo shirika la Amnesty International limesema serikali inapaswa kuachana na mpango huo wa aibu katika historia ya kisiasa ya Uingereza.
Mpango huo wa Rwanda umeigharimu serikali ya Uingereza kiasi cha pauni zisizopungua milioni 140 katika malipo kwa Rwanda kabla ya hata kundoa ndege moja.
Kesi hiyo ilipelekwa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, ambazo zilisema kuwa mpango huo ulikuwa kinyume cha sheria kwa sababu Rwanda si "nchi salama." Serikali ilipinga uamuzi huo bila mafanikio katika Mahakama ya Juu Zaidi.
Serikali imesema mkataba mpya utakuwa tayari katika musa wa siku kadhaa na utachukuwa takribani wiki tatu kuidhinishwa na bunge kuwa sheria.