Waziri Mkuu wa zamani wa Mali afariki dunia akiwa kizuizini
22 Machi 2022Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Mali, mwenye umri wa miaka 68, alikamatwa na kisha kuwekwa chini ya waranti ya kukamatwa Agosti mwaka jana, kama sehemu ya uchunguzi wa kupambana na rushwa, unaohusishwa hasa na kandarasi za zana za kijeshi wakati alipokuwa Waziri Mkuu.
Hali ya afya yake ilikuwa imezorota sana kutokana na mazingira ya kuzuiliwa kwake. Soumelylou Boubeye Maiga, alikuwa amelazwa hospitalini takriban miezi mitatu iliyopita, lakini kuhamishwa kwake kwa matibabu, licha ya mapendekezo la madaktari wake, halikuweza kuruhusiwa na mamlaka ya mpito.
→Macron atarajiwa kuwaondoa wanajeshi wake Mali
Familia imekataa uchunguzi wa maiti
Abdina Karembe, mwenyekiti wa tawi la vijana la chama cha CFP, cha waziri mkuu huyo wa zamani amesema kiongozi wao amefariki kutokana na huduma mbovu ya matibabu.
''Aliteswa sana, na hatutaki tena kuutesa mwili wake kwa sababu viongozi wameomba kuweko na uchunguzi wa maiti ilikufahamu chanzo cha kifo chake. Familia imeamua kuwa haiitaji uchunguzi huo. Mazingira ya kushikiliwa kwake yalikuwa magumu kila mtu amefahamu hilo.''
Serikali ilitoa taarifa baadaye Jumatatu ikitangaza kwamba Maiga alikufa baada ya ugonjwa wa muda mrefu na kuwasilisha rambirambi kwa familia.
''Anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa hili''
Kwenye mtandao wake wa Twitter, Rais wa Niger Mohamed Bazoum alisema kunyimwa huduma ya matibabu nje ya nchi kwa Maiga ilikuwa sawa na mauaji. Huku akilinganisha kifo cha Maiga sawa na kile cha Rais Modibo Keita mwaka 1977 ambaye pia alifariki akiwa gerezani. Ujumbe huo umekosolewa vikali na utawala wa Bamako.
Aboubacar Sidick Fomba, mjumbe wa Baraza la Kitaifa la Mpito la Mali (CNT), amesema Rais wa Niger Mohamed Bazoum ni kibaraka cha Wafaransa na ambaye anastahili kufunguliwa mashtaka kwa maoni yake hayo.
''Tunatoa wito kwa mamlaka ya kipindi cha mpito kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Rais wa Niger Mohamed Bazoum. Kwa sababu akizungumzia mauaji, hiyo inamaanisha kwamba ana uthibitisho. Na, tunatarajia atuletee ushahidi huo. Anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa hili."
Maiga, aliyekuwa waziri wa ulinzi, aliteuliwa kuwa waziri mkuu mnamo 2017 na kujiuzulu miaka miwili baadaye, wiki nne baada ya mauaji ya wafugaji wapatao 160 wa kabila la Fulani yaliyofanywa na kikundi wanamgambo waliojiita walinda haki.