1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto kurejea nyumbani

Tuma Provian Dandi17 Oktoba 2007

Baada ya kipindi kirefu cha kuishi uhamishoni, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Bibi Benazir Bhutto amethibitisha kutaka kurejea nyumbani

https://p.dw.com/p/C7hN
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Bibi Benazir Bhutto
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Bibi Benazir BhuttoPicha: AP

Akiwahakikishia waandishi wa habari mjini Dubai kuhusu uamzi wake, Waziri Mkuu wa Pakistan Bibi Benazir Bhutto amesema yuko tayari kurejea nyumbani hapo kesho baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka minane kutokana na sababu za kisiasa.

Ameendelea kueleza kwamba anamwomba Mungu arejeshe demokrasia na maisha ya amani nchini Pakistan baada ya kuparaganyika kutokana na vita pamoja mashambulizi mbalimbali yanayofanywa na wafuasi wa mitandao ya kigaidi.

Pamoja na uamzi wa mwanasiasa huyo kutaka kurejea nyumbani serikali bado inamwekea shinikizo la kutorejea nchini mwake hadi hapo Mahakama Kuu itakapotoa uamzi wa kumhalalisha Jenerali Perves Musharraf kama kweli anastahili kuwa Rais kisheria.

Bibi Bhutto aliyekuwa mtendaji wa serikali iliyopita kabla ya Rais Musharraf kuingia madarakani kwa njia ya mapinduzi, alilazimika kukimbia nchi kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi ya utendaji wake, vikiwemo visa vya ufisadi.

Pamoja na kutaka kurejesha nyumbani Bibi Bhutto anakabiriwa na hatarai nyingine kutoka kwa wanamgambo wanaosemekena kuwa na ushirikiano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, kwa kuwa walishatangaza azma ya kumuuwa, pamoja na Rais Perves Musharraf mwenyewe.

Mmoja wa watu wa karibu na Bibi Bhutto anayejulikana kwa jina la Mohammad Akram Farooqui, amesema kiongozi wake amejiandaa kwa hali yoyote itakayomtokea mara baada ya kurejea Mjini Karachi kusini mwa Pakistan.

Akiwa uhamishoni katika Falme za Kiarabu, Bibi Benazir Bhutto alikuwa rais wa chama cha siasa cha Pakistan Peoples’ Party-PPP.

Pamoja na kwamba anasubiri uamzi wa Mahakama Kuu ya Pakistan kumwidhinisha kuwa Rais, tayari Jenerali Musharraf ameshatangaza msamaha dhidi ya tuhuma zinazomkabiri Waziri Mkuu huyo wa zamani, lakini amemsihi kutorejea nyumbani hadi pale atakapopewa madaraka kamili baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu.

Akizungumzia kuhusu msamaha huo, Waziri Mkuu wa Pakistan Bwana Shaukat Aziz, amesisitiza kwamba Bibi Bhutto yuko huru kujea katika nchi yake na kwamba atachukuliwa kama raia mwingine mwenye dhamana na nchi yake, lakini asubiri hadi Rais Perves Musharraf atakapopewa madaraka kamili.

Nacho chama cha Bibi Benazir Bhutto, kimesema huenda mapokezi yake yatahudhuriwa na zaidi ya watu milioni moja ambao ni wafuasi wake, na kwamba watapita katika mitaa mbalimbali ya mji wa Karachi wakati wakienda kumpokea kwenye uwanja wa ndege.

Mkuu wa chama cha PPP katika jimbo la Sindh Bwana Qaim Ali Shah, amesema wafuasi wao wameanza kujiandaa kwenda kumlaki kiongozi wao na kwamba wengi wameshakata tiketi za magari na treni kwa ajili hiyo wakati wengine watatumia usafiri wao wa binafsi.

Wakati kiongozi huyo akitaka kurejea nyumbani kutoka uhamishoni, ripoti nyingine kutoka Pakistan inaeleza kwamba Rais Perves Musharraf anazidi kupoteza umaarufu wake kutoka na sera zake zinazopingwa na baadhi ya wananchi wa Pakistan.