1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza ajiuzulu ubunge.

10 Juni 2023

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Boris Johnson ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya ubunge na ameshutumu uchunguzi wa bunge juu ya kashfa ya "Partygate" kwa kudai walitaka kumfukuza.

https://p.dw.com/p/4SPrN
UK, London | Boris Johnson
Picha: Victoria Jones/PA Wire/empicspicture alliance

Johnson mwenye umri wa miaka 58, amesema anajiuzulu mara moja kama mbunge wa Tory na kulazimisha kufanyika kwa uchaguzi mdogo ili kujaza nafasi yake.

Kujiuzulu kwake kumefungua tena mgawanyiko katika chama tawala cha Conservative kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alikuwa akipigania mustakabali wake wa kisiasa katikati ya uchunguzi wa bunge kuhusu iwapo alilipotosha bunge aliposema sheria zote za kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona zilifuatwa wakati wa kuandaa sherehe katika afisi yake ya Downing Street wakati nchi hiyo ilipokuwa chini ya vizuizi vya Corona.

Kamati ya bunge iliyokuwa inamchunguza ilikuwa na uwezo wa kupendekeza Johnson asimamishwe bungeni kwa zaidi ya siku 10 iwapo wangebaini kuwa alilipotosha bunge, na kufungua mwanya wa kufanyika kwa uchaguzi mdogo.