1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Brexit David Davis ajiuzulu

Caro Robi
9 Julai 2018

Waziri anayesimamia mchakato wa Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya- Brexit, David Davis, na naibu wake wamejiuzulu kutokana na mpango wa kudumisha mahusiano ya karibu ya kiuchumi na Umoja huo.

https://p.dw.com/p/313sI
Rücktritt Brexit-Minister David Davis
Picha: Reuters/H. McKay

Macho yote sasa yanaelekezwa kuona kama kuna mawaziri wengine walio na msimamo mkali kuhusu mchakato huo wa Brexit watakaojiuzulu baada ya Davis kusema amechukua hatua hiyo kumzuia May kuupa Umoja wa Ulaya nguvu zaidi katika mazungumzo yanayoendelea.

Davis, ambaye alifanya kampeni mwaka 2016 wakati wa kura ya maoni kuunga mkono Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya, ameiambia redio ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, kuwa makubaliano yaliyofikiwa na baraza la mawaziri linaloongozwa na Waziri Mkuu Theresa May, linawapa maafisa wa Umoja wa Ulaya wanaosimamia mashauriano ya mchakato wa Brexit nguvu zaidi na kwa njia rahisi na anahofia maafisa hao watataka matakwa mengi zaidi kutimizwa.

Je, mawaziri zaidi watajiuzulu?

Kujiuzulu kwa waziri huyo na naibu wake, Steve Baker, ni pigo kwa May ambaye Ijumaa iliyopita alionekana kufikia muafaka na mawaziri wake ambao wamegawanyika vibaya kuhusiana na suala hilo la Brexit.

Belgien EU-Gipfel in Brüssel | Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/AFP/L. Marin

Hatua ya Davis na manung'uniko yanayoendelea miongoni mwa mawaziri, yanaibua maswali kuhusu iwapo May ataweza kulishawishi bunge ambalo nalo limegawika kuhusu mapendekezo yake juu ya mustakabali wa Uingereza baada ya Brexit.

Kujiuzulu kwa Davis aliyeteuliwa miaka miwili iliyopita kuongoza mchakato wa Brexit pia kutayatatiza mazungumzo magumu ya Brexit, ikiwa imesalia miezi tisa tu kabla ya Uingereza kujiondoa rasmi kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Katika barua iliyotumwa kwa May mapema leo asubuhi, Davis amesema hayuko tayari kutii maagizo ambayo hayaamini juu ya msimamo wa May kuhusu mazungumzo ya Brexit ambayo yatapelekea Uingereza kufuata kila kitu Umoja wa Ulaya unataka.

Akijibu barua hiyo, May amesema hakubaliani na mtizamo wa Davis lakini amemshukuru kwa kazi aliyoifanywa alipokuwa waziri wa Brexit. Waziri huyo mkuu wa Uingereza anatarajiwa leo mchana kulihutubia bunge ili kuliarifu kuhusu mapendekezo yake ya kushirikiana na Umoja wa Ulaya baada ya Brexit kuhusu biashara.

Waziri wa mambo ya nje Boris Johnson, mmoja wa viongozi walio katika mstari wa mbele kutaka Uingereza kujitenga kikamilifu na Umoja wa Ulaya, amekuwa akipinga mapendekezo ya May lakini mpaka sasa, tangu Ijumaa iliyopita hajatoa tamko lolote hadharani kuhusu mtizamo wake ulipofika mchakato huo wa Brexit. May amemteua Dominic Raab kuwa waziri mpya wa Brexit.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef