1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa fedha Afrika Kusini avuliwa madaraka

31 Machi 2017

Hatua ya Jacob Zuma ya kumuondoa  waziri wake wa fedha Pravin Gordhan inaashiria mgawanyiko ndani ya chama kinachotawala cha ANC. Zuma pia anashinikizwa na vyama vya upinzani aondoke madarakani

https://p.dw.com/p/2aNov
Südafrika Finanzminister Pravin Gordhan
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. van Zuydam

Rais Jacob Zuma alipomfukuza kazi waziri huyo hapo jana usiku aliwateuwa mawaziri wapya kumi kwenye baraza lake lenye mawaziri 35.  Hali ya sasa nchini Afrika Kusini inaashiria mpasuko katika chama kinachotawala cha ANC hasa miongoni mwa wanachama wa ngazi za juu waliopigania uhuru wa nchi hiyo na kuweza kuingia madarakani wakiongozwa na aliyekuwa rais wa kwanza mweusi Nelson Mandela.  Rais Zuma amemchagua aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Malusi Gigaba kuwa waziri mpya wa fedha.  Gigaba hajulikani sana na pia hana uzoefu katika mambo ya fedha.  Wizara zilizofanyiwa mabadiliko ni pamoja na za nishati ,mambo ya ndani na utalii baadhi ya mawaziri ni wapya na wengine wamehamishiwa kwenye wizara zingine. 

Südafrika Johannesburg Oppoosition EFF Julius Malema
Kiongozi wa chama cha EFF Julius MalemaPicha: picture-alliance/dpa/C. Tukiri

Wakati huo huo chama cha mrengo wa shoto nchini humo cha EFF kimewasilisha maombi rasmi katika mahakama ya juu ya katiba. Kinataka Zuma afunguliwe mashtaka ili aondolewe madarakani. Kiongozi  wa chama hicho Julius Malema amesema Zuma hana uwezo wa kuongoza kutokana na kuhusishwa na kashfa kadhaa za rushwa. Nacho chama kikuu cha upinzani cha Democratik Alliance pia kimesema kitawasilisha bungeni muswada wa kutokuwa na imani na rais Zuma kutokana na kushindwa kwake kuushughulikia uchumi unaozidi kuwa mbaya na kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wasiokuwa na ajira nchini humo.

Hatua ya rais Zuma ya kumfukuza waziri wake wa fedha haikupokewa vyema na wawekezaji ambao walimwona Gordhan kuwa ni mtu mwaminifu aliyejitolea kupambana na rushwa, ubadhirifu wa fedha za serikali pamoja na lengo lake la kutaka kupunguza nakisi katika bajeti ya Afrika Kusini.  Kufikia jana jioni sarafu ya Randi ilipungua thamani yake dhidi ya dola ya Marekani katika soko la hisa la bara Asia.  Hali hiyo ilianza kujitokeza tangu wiki iliyopita pale tetesi zilipozagaa kwamba Zuma alipanga kumvua madaraka waziri wake wa fedha na ilidhihirika pale alipomtaka waziri huyo kukatiza ziara yake nchini Uingereza na kurejea nyumbani mara moja. Gordhan alikuwa Uingereza katika ziara ya kuvutia biashara na  vitega uchumi zaidi.

Mwandishi:  Zainab Aziz/AFPE/dw.com/p/2aNYe

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman