Waziri wa mambo ya kigeni wa Korea Kaskazini azuru Sweden
16 Machi 2018Ziara hiyo imeibua uvumi wa uwezekano wa mkutano baina ya rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un. Waziri Ri Yong Ho, aliwasili katika uwanja wa ndege wa Stockholm Arlanda akitumia ndege ya moja kwa moja kutoka Beijing alhamis jioni, na kutumia masaa kadhaa katika wizara ya mambo ya nje ya Sweden kabla ya kurudi katika ubalozi wa Korea Kaskazini.
Wizara ya mambo ya nje ya Sweden imesema katika taarifa yake kwamba mazungumzo hayo "yatalenga wajibu wa kibalozi wa Sweden katika kuilinda Marekani, Canada na Australia", lakini pia itagusia hali ya usalama katika rasi ya Korea. Iliongeza kwamba taarifa ya pamoja ya mazungumzo hayo itatolewa siku ya Ijumaa baada ya mazungumzo ya mawaziri hao wawili. Siku ya Ijumaa, Ri alikutana kwa muda mfupi na waziri mkuu Stefan Lofven katika makao makuu ya serikali ya Sweden. Maelezo ya mazungumzo yao nayo hayakutolewa, wakati waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini akizuru Stockholm ambako aliwahi kuwa mwanadiplomasia katika ubalozi.
Sweden imekuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Korea Kaskazini tangu mwaka 1973 na ni mojawapo ya mataifa machache ya magharibi ambayo yana ubalozi wake mjini Pyongyang. Inatoa huduma za kibalozi kwa ajili ya Marekani nchini Korea Kaskazini. Naye mkuu wa utumishi wa rais wa Korea Kusini Im Jong-seok amesema watatuma ombi la kufanyika mkutano wa ngazi ya juu baina ya viongozi wa mataifa hayo jirani."Kamati ya maandalizi imeamua kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu baina ya Korea Kusini na kaskazini mwishoni mwa mwezi Machi kuandaa mkutano wa kilele kati ya Korea mbili, na tutapendekeza rasmi mazungumzo hayo kwa Korea Kaksazini, alisema Im Jong-seok.
Hayo yakiendelea, Korea Kusini na Marekani zimesema zitapunguza mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya kila mwaka katika kurekebisha uhusiano wa kidiplomasia na Pyongyang.
Mazoezi hayo yanayofanywa kila mwaka msimu wa machipuko, kwa kawaida huikasirisha Korea Kaskazini iliyojihami kwa silaha za nyukilia, na ambayo inazituhumu nchi hizo kwamba zinafanya maandalizi ya kuivamia na kujibu kwa kufanya uchokozi wa aina yake na kuchochea mvutano.
Mazoezi ya pamoja yalicheleweshwa ili kuepuka kuingiliana na michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi iliyofanyika mjini Pyeongchang huko Korea Kusini mwezi uliopita.
Lakini kwa mujibu wa afisa mwandamizi katika ofisi ya rais mjini Seoul, Kim aliueleza ujumbe wa Korea Kusini uliotembelea nchini humo mwezi uliopita kwamba "ataelewa" kama mazoezi hayo yataendelea.
Shirika la habari la Korea Kusini Yonhap, limenukuu chanzo kimoja kutoka jeshi kikisema mazoezi hayo ya Foal Eagle, mazoezi yanayohusisha makumi kwa maelfu ya majeshi, yataanza mapema mwezi Aprili lakini yatafupishwa kutoka miezi miwili hadi mmoja.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga