Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mattis ajiuzulu
21 Desemba 2018Uamuzi wa kujiuzulu Jim Mattis, umejiri baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutangaza anawahamisha "idadi kubwa ya wanajeshi wa Marekani kutoka Afghanistan na umesadifu pia siku moja baada ya tangazo lake la kuwaondowa wanajeshi waliowekwa nchini Syria. Maamuzi yote hayo mawili yamekosolewa na jumuia ya kimataifa. Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Florence Parly ameutaja uamuzi wa rais Trump wa kuwaondowa wanajeshi wa Marekani nchini Syria kuwa ni "uamuzi wenye madhara makubwa.""Hatukubaliani na hoja kwamba wafuasi wa itikadi kali wa dola la kiislam wameshindwa nguvu nchini Syria-amesema. Parly amemsifu wakati huo huo waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis na kumtaja kuwa "mwanajeshi shujaa" na mshirika mkubwa."
Wanajeshi hadi 14.000 wa Marekani kuhamishwa Afghanistan
Jim Mattis anaetajwa kuwa mwanasiasa wa serikali ya Marekani anaeheshimiwa zaidi katika majukwaa ya kisiasa ataacha wadhifa wake mwishoni mwa mwezi wa february baada ya miaka miwili ya juhudi za kumtanabahisha rais Trump aregeze msimamo wake shupavu. Katika barua yake ya kujiuzulu, Jim Mattis amemwambia rais Trump kwamba anajiuzulu ili ampate "mtu atakaekuwa na msimamo unaolingana na wake."
Vyombo vya habari vya Marekani vimenukuu duru za kuaminika zikisema rais Trump ameshaamua kuwaondowa pia wanajeshi kati ya 7000 na 14.000 waliowekwa Afghanistan.Tangazo hilo la ghafla lililotolewa katika wakati ambapo "mazungumzo ya suluhu kati ya Marekani na wataliban wa Afghanistan yamekuwa yakiendelea wiki hii mjini Abu Dhabi ,limewashangaza wahusika mjini Kabul. Hata hivyo rais wa Afghanistan Ashraf Ghani anasema uamuzi huo hautoathiri hali ya usalama nchini mwake.
Marco Rubio atahadharisha dhidi ya njia mbaya inayofuatwa
Wanasiasa kadhaa wa Republican wameelezea masikitiko yao kwa uamuzi wa kujiuzulu Waziri wa Ulinzi Jim Mattis. "Ndio kwanza nimesoma barua ya kujiuzulu Jenerali Mattis," ameandika katika mtandao wake wa Twitter Seneta wa Florida Marco Rubio, aliyesema tunanukuu: "Ni dhahiri kwamba tunaelekea kufuata makosa kadhaa ya kisiasa ambayo yataihatarisha nchi yetu, yatavuruga mafungamano yetu na kuwapa nguvu maadui zetu." Mwisho wa kumnukuu Marco Rubio.
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Khelef