1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Ulinzi wa Pakistan azuiwa kusafiri nje ya nchi

18 Desemba 2009

Ni kutokana na kuhusishwa na tuhuma za rushwa.

https://p.dw.com/p/L73r
Waziri wa Ulinzi wa Pakistan Chaudry Ahmed Mukhtar, ambaye amezuiwa kusafiri nje ya nchi hiyo.Picha: AP

Siku moja tu baada ya Mahakama Kuu nchini Pakistan kufuta msamaha uliokuwa unawalinda wanasiasa wasishtakiwe, uamuzi wa mahakama hiyo wa kuzirejesha kesi za zamani zilizokuwa zinawakabili wanasiasa wa ngazi ya juu umeanza kutishia uimara wa serikali ya nchi hiyo, baada ya jana jioni Waziri wa Ulinzi kuzuiwa kusafiri kutokana na tuhuma za rushwa.

Taasisi ya juu ya nchi hiyo inayoshughulika na masuala ya rushwa iliagiza kuwekwe marufuku ya kusafiri kwa zaidi ya watu 250 kutokana na makosa ya zamani ya rushwa, tangu Mahakama Kuu nchini humo hapo jana ilipoamua kufuta msamaha uliokuwa unawalinda wanasiasa wasishtakiwe, akiwemo Rais Asif Ali Zardar.

Hatua ya mahakama hiyo imesababisha mgongano katika serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Marekani, huku upande wa upinzani ukidai Rais wa nchi hiyo Asif Ali Zardar ajiuzulu pamoja na mawaziri wanaohusishwa na tuhuma za rushwa.

Waziri wa Ulinzi wa Pakistan Ahmed Mukhtar, aliiambia televisheni moja ya nchini humo kwamba, alikuwa anatakiwa kufanya ziara ya kikazi nchini China, lakini jina lake limewekwa katika orodha ya watu ambao hawatakiwi kusafiri.

Mukhtar alikiambia kituo cha televisheni cha Geo kwamba alitakiwa kuwa nchini China kwa muda wa siku tatu, kujadiliana juu ya ununuzi wa manowari, lakini maafisa wake walipofika uwanja wa ndege waliambiwa ujumbe huo unatakiwa kusafiri bila ya waziri huyo.

Waziri huyo alisema alitaarifiwa na idara ya uchunguzi ya nchi hiyo kwamba jina lake lipo katika orodha hiyo, na maafisa wa idara hiyo walimwambia kuwa hawezi kuondoka nchini humo.

Taasisi ya Taifa ya Uwajibikaji ilisema iliiagiza wizara ya mambo ya ndani kuorodhesha majina ya watu 253 ambao hawatakiwi kusafiri nje ya nchi.

Afisa habari wa taasisi hiyo Naveed Satar, alisema orodha hiyo inahusisha wanasiasa, maafisa wastaafu wa jeshi na baadhi ya wanadiplomasia.

Alisema baadhi ya hati za kukamatwa ambazo zilitolewa zamani zimerejewa tena, na mali za wanaotuhumiwa zimekamatwa.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema jina la rais Zardar liliondolewa kwa sababu ana kinga ya rais, lakini jina la waziri wa mambo ya ndani Rehman Malik pia lipo katika orodha hiyo.

Balozi wa Pakistan nchini Marekani Husain Haqqan, alitoa wito kwamba kufutwa kwa msamaha huo kusiiyumbishe nchi, ambayo ipo kwenye shinikizo kubwa la Marekani, inayoitaka nchi hiyo kuongeza juhudi zaidi katika kupambana na wanamgambo wa kiislamu katika mpaka na Afghanistan.

Pakistan ipo katika nafasi ya 40 katika orodha ya nchi 180 zinazoangaziwa na shirika la kimataifa la kupamabana na rushwa la Transparency International, na serikali nyingi zimeanguka na nyingine kupinduliwa na jeshi kutokana na tuhuma za rushwa.

Msamaha huo uliidhinishwa mwaka 2007 na rais wa zamani wa nchi hiyo Pervez Musharaf, aliyekuwa anakabiliwa na shinikizo la kuitisha uchaguzi ili kumaliza kipindi cha miaka minane ya utawala wa kijeshi.

Mwandishi:Lazaro Matalange/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman