Weinstein ashtakiwa kwa ubakaji na makosa ya kingono
25 Mei 2018Tajiri wa Hollywood, Harvey Weinstein, alikamatwa na kushtakiwa siku ya Ijumaa kwa makosa wa ubakaji na uhalifu wa kingono dhidi ya wanawake wawili, karibu miezi minane baada ya kuibuka kwa kashfa kuhusu madai ya dhulma za kingono yaliozaa Vuguvugu la #MeToo.
Kigogo huyo wa zamani - aliyekuwa akihusudiwa zaidi mjini Hollywood na ambaye filamu zake zilishinda tuzo kadhaa za Oscar - alisindikizwa kutoka kituo cha polisi cha Manhattan akiwa kwenye pingu na kufikishwa mahakamani siku ya Ijumaa.
Zaidi ya wanawake 70 wamemshutumu mwasisi huyo mwenza wa studio za filamu za Miramax na kampuni ya Weinstein, kwa makosa ya kingono yakiwemo ya ubakaji, huku tuhuma nyingine zikidaiwa kutendeka miongo kadhaa iliyopita.
Mwenyewe amekanusha kufanya ngono na mtu yeyote bila ridhaa yake na wakili wake, Benjamin Brafman, amesema atakanusha mashtaka hayo anayodaiwa kutenda mwaka 2003 na 2004.
"Bwana Weinstein atatoa maelezo ya kutokuwa na hatia," Brafamn aliwaambia waandishi habari nje ya mahakama ya Manhattan ambako mteja wake alifikishwa kwa muda mfupi mbele ya jaji kabla ya kuomba dhamana.
"Tunadhamiria kwenda haraka sana ili kutupilia mbali mashtaka hayo. Tunaamini kwamba yana kasoro kikatiba. Tunaamini kwamba hayaungwi mkono na ushahidi."
Tuhuma dhidi ya Weistein zilizoripotiwa kwa mara ya kwanza na magazeti ya New York Times na New Yorker mwaka uliopita, zilipelekea kuanzishwa kwa vuguvugu la #MeToo ambamo mamia ya wanawake wamewatuhumu waziwazi wanaume wenye nguvu katika sekta za biashara, serikalini na burudani kwa kuwadhalilisha.
Mwandishi: Iddi Ssessanga
Mhariri: Mohammed Khelef
Weinstein mwenye umri wa miaka 66, anashtakiwa kwa makosa mawili ya ubakaji na moja na uhalifu wa kingono dhidi ya wanawake wawili, wamesema waendesha mashtaka. Lakini hawakutambulisha wanawake hao.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.
Mhariri: Mohammed Khelef