Werner: "Afadhali kucheza nje kuliko Bayern"
2 Mei 2020Werner, mchezaji wa safu ya ushambuliaji wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani, Die Mannachaft, ana mkataba na Leipzig hadi 2023 lakini inaripotiwa anaweza kuondoka kwa kitita cha euro miliono 60 msimu wa kiangazi.
Bayern wanasemekana walimtaka mwaka 2019 lakini makubaliano hayakuafikiwa, wakati Bayern walipoamua kuelekeza nguvu zao kwa winga wa timu ya taifa ya Ujerumani, Leroy Sane, anayesakata ngozi na klabu ya Manchester City katika ligi ya Premier huko England.
Vinara wa ligi ya Premier Liverpool na Chelsea ni miongoni mwa vilabu ambavyo pia vinamnyatia Werner mwenye umri wa miaka 24. Werner ameliambia gazeti la Bild la hapa Ujerumani kwamba uwezekano wa kuhamia katika klabu ya Bundesliga haupo.
"Bayern ni klabu kubwa, hatuhitaji kulizungumzia hilo. Na Hansi Flick amethibitisha msimu huu kwamba ni kocha mzuri kweli kweli. Lakini iwapo uhamisho litajitokeza kuwa suala muhimu, basi afadhali nihamie nje ya nchi badala ya kujiunga na Bayern," alisema Werner.
"Ni kwamba kuwa na changamoto katika ligi nyingine kungenivutia mimi zaidi kuliko uhamisho ndani ya Bundesliga." akaongeza.
Werner pia amesema shukran na utambuzi wa kuheshimiana ni kigezo muhimu jambo ambalo halikujitokeza mwaka jana kwa Bayern huku akisema "Siwezi kujibu ni kitu gani kilichoipa msukumo Bayern wakati huo." Hata hivyo Werner aidha amesema hana nia ya kuipa kisogo timu yake ya RB Leipzig, ambayo imetinga duru ya robo fainali ya kombe la mabingwa barani Ulaya, Champions League, msimu huu wa joto kwa vyovyote vile.
"Nashukuru sana nilichonacho katika klabu ya RB Leipzig na kwa hivyo singeweza kusema kabisa: "Lazima kabisa niondoke klabu hiyo!" alisema.
(dpae)