1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado hakuna suluhu kwa mzozo wa Gaza

Josephat Nyiro Charo21 Novemba 2012

Mashambulizi ya angani ya jeshi la Israel yameutikisa Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo (21.11.2012) huku maroketi ya Hamas nayo yakipiga upande wa Israel.

https://p.dw.com/p/16n6T

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alikutana na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu jana mjini Jerusalem katika jitahada za kutuliza hali huko Gaza. Westerwelle alisema Israel ina haki ya kuwalinda raia wake dhidi ya mashambulizi ya makombora kutoka Gaza akisema "Tujitahidi kuhakikisha mapigano yanasitishwa."

Awali Westerwelle alikutana na rais wa Israel, Shimon Peres na kuihimiza Misri itumie nafasi yake kuhakikisha makubaliano ya kusitisha mapigano yanasitishwa. Peres ameishukuru Ujerumani kwa juhudi zake za upatanishi akisema Israel inathamini msaada wa kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, mmoja wa viongozi wenye dhima kubwa katika Umoja wa Ulaya.

Mashambulizi ya angani ya Israel yameendelea kuutwanga Ukanda wa Gaza katika usiku mwingine wa machafuko. Ripoti zinasema uharibifu mkubwa umetokea katika maeneo mbalimbali ya Gaza na mashirika kadhaa ya habari yameathirika. Wapalestina takriban 130 wameuwawa tangu mapigano yalipozuka wiki moja iliyopita. Waisraeli watano pia wameuwawa kutokana na mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza.

Clinton akutana na Netanyahu

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, aliwasili katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Jerusalem akitokea Phnom Penh, Cambodia na kwenda moja kwa moja kukutana na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu jana usiku. Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari Clinton aliapa kuulinda usalama wa Israel huku akitoa mwito mapigano katika Ukanda wa Gaza yasitishwe haraka.

"Katika siku zijazo Marekani itashirikiana na washirika wetu nchini Israel na pia katika eneo zima kufikia muafaka unaoimarisha usalama kwa Waisraeli, kuboresha hali kwa watu wa Gaza na kuelekea amani ya pamoja kwa watu wote wa eneo hili."

Clinton alimwambia Netanyahu kwamba Marekani iko ngangari kuulinda usalama wa Israel na wala haitatetereka. Hata hivyo alisitiza kwamba hiyo ndiyo sababu kwa nini wanaamini ni muhimu kutuliza hali ya mambo katika maeneo ya Wapalestina.

Israel's Prime Minister Benjamin Netanyahu and U.S. Secretary of State Hillary Clinton deliver joint statements in Jerusalem November 20, 2012. The United States signalled on Tuesday that a Gaza truce could take days to achieve after Hamas, the Palestinian enclave's ruling Islamist militants, backed away from an assurance that it and Israel would stop exchanging fire within hours. REUTERS/Baz Ratner (JERUSALEM - Tags: POLITICS CIVIL UNREST TPX IMAGES OF THE DAY)
Bado hali ni tete Ukanda wa GazaPicha: Reuters

Netanyahu kwa upande alimwambia Clinton kuwa yuko tayari kukubali suluhisho la muda mrefu ili mradi mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza yanakoma. "Kama suluhisho la muda mrefu linaweza kupatikana kwa njia ya kidiplomasia, basi Israel itakuwa mshirika wa suluhisho la aina hiyo."

Hata hivyo Netanyahu ameonya kwamba ikiwa harakati nzito ya kijeshi itahitajika kuzuia mfululizo wa mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza, Israel haitasita kufanya inachohitajika ili kuwalinda raia wake.

Juhudi za upatanishi zaendelea

Wapatanishi wa kimataifa wamekuwa mbioni kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano na kuepusha operesheni ya ardhini ya jeshi la Israel. Kufikia sasa juhudi zote zimefeli. Wapatanishi walidokeza awali kuwa makubaliano yangetangazwa mjini Cairo, jana jioni kufuatia siku kadhaa za mashauriano yaliyosimamiwa na utawala mpya wa kiislamu wa Misri.

Waziri Clinton amedokeza kuwa tangazo lolote la kusitishwa kwa mapigano litatolewa atakapokamilisha ziara yake mjini Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan na mjini Cairo Misri.

Israel's Prime Minister Benjamin Netanyahu and U.S. Secretary of State Hillary Clinton deliver joint statements in Jerusalem November 20, 2012. The United States signalled on Tuesday that a Gaza truce could take days to achieve after Hamas, the Palestinian enclave's ruling Islamist militants, backed away from an assurance that it and Israel would stop exchanging fire within hours. REUTERS/Baz Ratner (JERUSALEM - Tags: POLITICS CIVIL UNREST TPX IMAGES OF THE DAY)
Hillary Clinton (kulia) na Benjamin NetanyahuPicha: Reuters

Clinton akutana na Abbas

Tayari Clinton amekutana na rais wa mamlaka a ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, huko Ramallah. Wanaharakati takriban 50 walikusanyika nje ya ikulu ya rais ambako viongozi hao walikuwa wakikutana kupinga ziara ya mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani. Clinton anatarajiwa baadaye leo kwenda Cairo kukutana na rais wa Misri, Mohammed Morsi. Kwa upande mwingine msemaji wa serikali ya Israel, Mark Regev, amesema hawezi kuthibitisha ripoti kwamba waziri huyo atakutana tena na Netanyahu.

Awali katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alikutana na Netanyahu mjini Jerusalem na kutoa mwito mapigano yasitishwe, akisema mzozo huo yumkini ukalitumbukiza eneo zima la Mashariki ya Kati katika hatari kubwa.

Mwandishi: Josephat Charo/Peter Kapern

Mhariri: Daniel Gakuba