WFP yatoa matumizi ya teknolojia katika maeneo kame Kenya
26 Julai 2024Mabadiliko ya tabia nchi yaliyoshuhudiwa kote ulimwenguni, yamewasukuma wafugaji wengi kutoka hapa jimboni Marsabit kugeukia kilimo kama njia mbadala ya kupata chakula cha kutosheleza familia zao. Kulingana na ripoti iliyotolewa na mamlaka ya kukabiliana na majanga nchini NDMA, asilimia 75 ya mifugo waliangamia hapa Marsabit wakati wa ukame misimu miwili iliyopita.
UN: Watu milioni 13 wanakabiliwa na njaa kubwa katika eneo la Pembe ya Afrika
Idadi kubwa ya wakaazi wa majimbo yenye ukame wamekuwa wakitegemea misaada ya vyakula kutoka serikali na mashirika ya kiutu. Hali hiyo ikionekana kuipa changamoto shirika la chakula duniani WFP ambalo limetangaza mpango wake wa kuwekeza katika teknolojia kuwezesha kilimo katika majimbo yenye ukame. Mkurugenzi wa WFP nchini Kenya Lauren Landis ameelezea umuhimu wa teknolojia kutumika kuboresha kilimo na utoshelevu wa chakula.
"Marsabit ni kama jangwa kwa namna fulani lakini tunaweza kuendeleza kilimo iwapo tutatumia teknolojia za kisasa. Kwa sasa tunazingatia kutumia teknolojia bora zaidi na vifaa vya kisasa kwa sababu tuna raslimali kwa haya yote,” alisema Landis.
WFP yatoa vifaa vya kutathmini ubora wa chakula
Wakati huo huo, WFP imenunua vifaa vya kutathmini ubora wa vyakula baada ya kuwepo na shauku kuhusu usalama wa vyakula vinavyoingizwa nchini kutokea taifa jirani la Ethiopia. Naibu gavana wa Marsabit Solomon Riwe akitaja upana wa mpaka wa Kenya na Ethiopia kuwa tishio kubwa kwa usalama wa vyakula vinavyotumika jimboni hapa.
"Tuna mpaka mmoja tu ambao ni rasmi nao ni Moyale lakini kutoka Moyale hadi Illeret ni ndefu sana kwa sababu unaweza kuingia Ethiopia na kutoka bila kujulikana, Kama hatutachunga,tunaweza kuathirika.”
WFP inahitaji dola milioni 400 kuwalisha mamilioni ya watu wanaohitaji msaada Barani Afrika
Haya yanajiri wakati wafugaji katika maeneo bunge ya Laisamis, Moyale, Saku na Horr Kaskazini wakiendeleza kilimo biashara. Rahma Ahmed kutoka Dirdima kule Moyale akieleza kwamba, ukulima umesaidia kupunguza dhulma majumbani kwani wanawake wana uwezo wa kulisha familia zao kupitia kilimo.
"Zamani tulikuwa wafugaji lakini kwa wakati huu tunaendeleza shuguli za kilimo.hatuhitaji kuwasumbua waume zetu kwa sababu pesa tunazopata tunaweza kuwalipia watoto karo za shule,” alisema Rahma.
Kumekuwepo na miito mbalimbali kwa wafugaji kuanza kukumbatia kilimo kufuatia athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa wafugaji wengi nchini Kenya.