WFP: Msaada wa chakula wafikishwa Tigray
16 Novemba 2022Kurejeshwa kwa misaada katika jimbo la Tigray ilikuwa sehemu muhimu ya makubaliano yaliyotiwa saini nchini Afrika Kusini ya kusitisha vita katika mzozo wa miaka miwili ambao umeua watu wasiohesabika na kusababisha mgogoro wa kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia. soma Mkataba wa amani waafikiwa kati ya Ethiopia na TPLF
Aidha tangazo la WFP linajiri siku moja baada ya msafara wa misaada ya kimatibabu kutoka Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) kuingia Tigray, malori ya kwanza ya kuwasili katika eneo hilo kufuatia makubaliano kati ya serikali ya Ethiopia na Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).
Kupitia mtandao wa kijamii, shirika hilo limechapisha taarifa hiyo huku msemaji wake akiliambia shirika la habari la AFP kwamba malori 15 yaliingia katika eneo hilo siku ya Jumatano, na mengine zaidi yanatarajiwa katika siku zijazoulikuwa huu ukiwa msaada wa kwanza kuwasili katika eneo hilo tangu makubaliano ya kusitisha mapigano ya Novemba 2.
soma Ethiopia na Tigray wakubaliana kusitisha moja kwa moja mapigano
Shirika hilo lilisema msafara huo uliingia Tigray kupitia nchi jirani ya Amhara kwa mara ya kwanza tangu Juni 2021, wakati wapiganaji wa Tigray walipoukamata tena mji huo kutoka mikononi mwa vikosi vya serikali na kupanua wigo wake hadi katika mikoa ya mpaka ya Amhara na Afar.
Utekelezaji makubaliano
Makubaliano ya Novemba 2 yalifuatiwa na makubaliano ya utekelezaji yaliyofikiwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi siku ya Jumamosi, na pande hizo mbili zikijitolea kuwezesha upatikanaji wa haraka wa msaada wa kibinadamu kwa wote wanaohitaji huko Tigray na mikoa jirani kutekelezwa mara moja.
Katika mkutano huo Jenerali Tadesse Werede, kamanda mkuu wa vikosi vya Tigray alisema "Tumeteseka sana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na bado tunaendelea kuteseka. Ahadi tunayofanya leo ni ya matumaini na matarajio kwamba mateso ya watu wetu yatakwisha hivi karibuni."
soma Guterress: Hali inaendelea kuwa mbaya Ethiopia
Tigray, eneo lenye wakazi milioni sita, limekuwa likikabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula na dawa, pamoja na upatikanaji mdogo wa huduma muhimu zikiwemo za umeme, benki na mawasiliano, huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa watu wengi wako kwenye ukingo wa njaa.
AFP/Reuters