1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WFP yahofia vita vya Sudan kusambaa Afrika Mashariki kote.

30 Aprili 2023

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetahadharisha juu ya mapigano yanayoendelea nchini Sudan. Limesema vurugu hizo zinaweza kuzitumbukiza nchi zingine za eneo la Afrika Mashariki katika mgogoro wa kibinadamu.

https://p.dw.com/p/4Qj3N
Sudan Karthoum | Unruhen: Ausgebranntes Auto
Picha: EL TAYEB SIDDIG/REUTERS

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetahadharisha juu ya mapigano yanayoendelea nchini Sudan. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema vurugu hizo zinaweza kuzitumbukiza nchi zingine za eneo la Afrika Mashariki katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu.  Mkurugenzi wa WFP Martin Frick, ameliambia shirika la Habari la Ujerumani dpa kwamba theluthi moja ya wakazi wa Sudan walikumbwa na njaa hata kabla ya mapigano kuanza na sasa wanakabiliwa na mfumuko wa bei, uhaba wa bidhaa zote muhimu pamoja na chakula. Frick amesema nchi jirani za Chad na Sudan Kusini ambazo zimewapokea maelfu ya wakimbizi tangu mapigano yalipoanza nchini Sudan wiki mbili zilizopita, zinakabiliwa na ongezeko kubwa la kupanda kwa bei za bidhaa. Amesema bei za vyakula zimepanda kwa asilimia 28 katika kipindi cha muda mfupi na kwamba Shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani limelazimika kusitisha misaada yake kwa watu wapatao milioni 7.6 nchini Sudan kutokana na mapigano. Amesisitiza kuwa misaada itaendelea kuwafikia watu mara tu hali ya usalama itakaporejea.