WHO: Ugonjwa wa homa ya ini umewapata takriban watoto 200
26 Aprili 2022Jumla ya watoto 190 wanaougua ugonjwa huo ambao asili yake haijulikani wameorodheshwa na 140 kati yao wapo barani Ulaya.
Mkurugenzi wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa barani Ulaya, Andrea Ammon, amesema mjini Stockholm kwamba hadi sasa hakuna ushahidi unaoonesha kuwa ugonjwa huo unahusiana na safari za nje ya nchi na kwamba watoto wanaougua ugonjwa huo wengi wao walikuwa ni wenye afya njema hapo awali.
Ugonjwa huo wa homa ya ini wa aina yake ambao husababisha ini kushindwa kufanya kazi hadi mgonjwa kuhitaji huduma ya upandikizaji umeripotiwa katika nchi za bara la Ulaya, Israeli na Marekani.
Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, limesema angalau kifo kimoja kimeripotiwa kuhusiana na mripuko huo. WHO imesema watoto wenye umri wa kati ya mwezi 1 na miaka 16 ndio walioripotiwa kupata maradhi hayo.
Wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo unaweza kuhusishwa na virusi vinavyosababisha mafua lakini utafiti bado unaendelea.