1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaitisha mkutano kuujadili ugonjwa wa homa ya nyani

16 Agosti 2024

Shirika la Afya Duniani WHO leo limeitisha mkutano utakaojadili njia za kuhakikisha mgawanyo sawa wa vipimo, matibabu na chanjo za ugonjwa wa homa ya nyani,mpox.

https://p.dw.com/p/4jZ2l
Kongo I Mpox
Mgonjwa wa homa ya nyani, Mpox nchini Kongo.Picha: AP/picture alliance

Shirika la Afya Duniani WHO leo limeitisha mkutano utakaojadili njia za kuhakikisha mgawanyo sawa wa vipimo, matibabu na chanjo za ugonjwa wa homa ya nyani,mpox. Mkutano huo umeitishwa katika wakati wasiwasi unaongezeka wa kusambaa maradhi hayo ambayo WHO imeyatangaza kuwa dharura ya afya ya kimataifa.

Duru kutoka ndani ya WHO zimesema mkutano huo wa leo utawakutanisha wataalamu wa afya waliofanya kazi ya kuratibu mapambano ya janga la virusi vya Corona. Wataalamu hao wanajumuisha mashirika ya kimataifa na wakfu wa hisani kama Bill na Melinda Gates na asasi inayopigia debe upatikanaji chanjo kwa wote duniani ya Gavi. 

Soma zaidi. Pakistan na Sweden zripoti visa vya virusi va homa ya nyani

Watajadiliana namna ya kuhakikisha makosa yaliyojitokeza wakati wa kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19 hayajitokezi tena kwenye mlipuko wa sasa wa homa ya nyani. Hiyo ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya matibabu, madawa na chanjo. 

DR Kongo | Mpox (2024)
Mgonjwa wa homa ya nyani akipatiwa matibabuPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

Tayari WHO ilikwishautangaza ugonjwa wa homa ya nyani kuwa dharura ya kimataifa wiki hii baada ya mlipuko mkubwa ulianzia nchini Jamhuri ya KIdemokrasi ya Kongo kuanza kusambaa duniani. Sweden na Pakistan zimekuwa nchi za hivi karibuni kabisa kutangaza kuwa na wagonjwa wa mpox. 

Tangazo la WHO lilifuatia lile la kituo cha kupambana na magonjwa barani Afrika CDC ambacho kilitanga mpox kuwa kitisho kwa afya umma. Nchi kadhaa barani Afrika zimeripoti kupata wagonjwa wa homa ya nyani. Wikendi hii viongozi wakuu wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC  watakuwa na mkutano wa kilele nchini Zimbabwe na suala hilo huenda litakuwa ajenda ya kipaumbele. 

Viongozi hao 16 wa jumuiya ya SADC wanaendelea kuwasili mjini Harare na miito imetolewa ya kuliweka mezani suala la ugonjwa wa homa ya nyani. 

Mpox kwenye maeneo mapya

Ugonjwa wa homa ya nyani umekuwepo katika mataifa ya Afrika ya kati na magharibi kwa miaka mingi ingawa mara hii umegundulika katika maeneo mengine zaidi barani Afrika ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo haujawahi kabisa kuripotiwa.

Nchini Nigeria visa 39 vya ugonjwa huo wa homa ya nyani vimerekodiwa na tangu mwanzoni mwa mwaka huu,hayo yamesemwa na afisa wa afya ambaye ameonyesha wasiwasi wake juu ya kuongezeka na kuenea kwa ugonjwa huo duniani.

DR Congo |Mpox
Raia nchini kongo wakipewa elimu juu ya ugonjwa wa homa ya Nyani, MpoxPicha: Augustin Mudiayi/MSF/AP/dpa/picture alliance

Jide Idris ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Nigeria ameongeza kuwa  "Jumla ya kesi 39 zimethibitishwa kati ya kesi 788 zinazoshukiwa ingawa hakuna vifo vilivyorekodiwa,"

Soma zaidi. EU yazionya nchi zake zijiandae kwa wimbi la homa ya nyani

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ugonjwa huo unatajwa kuenea zaidi kuliko eneo lolote duniani. Samuel Roger, ni Waziri wa Afya nchini Kongo amesema.

"Takriban mikoa yetu yote kwa sasa imeathiriwa na virusi hivyo. Kulingana na ripoti ya hivi punde ya magonjwa, nchi yetu imerekodi visa 15,664 vinavyowezekana na vifo 548 tangu kuanza kwa mwaka huu."

Katika hatua nyingine  , Mamlaka ya afya barani Ulaya ECDC imeripoti kuwa bara la Ulaya litarajie kuathirika pia na homa hiyo kutokana na muingiliano wa watu wanaoingia barani humo kutoka maeneo mengine.

Taarifa hiyo inakuja saa chache baada ya kesi ya kwanza ya ugonjwa wa homa ya nyani kuthibitihswa nchini Sweden. Mamlaka hiyo sasa inapendekeza nchi za Ulaya kutoa ushauri kwa watu wanaosafiri kwenda au kurudi kuchukua tahadhari kutoka maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huo.