WHO yasema janga la maambukizi ya corona kuwa la muda mrefu
2 Agosti 2020Kamati ya shirika hilo la afya imekutana kwa mara ya nne ,tangu kulipuka kwa maambukizi miezi sita iliyopita na kupiga mbiu ya mgambo duniani kote. Kamati hiyo pia imetahadharisha juu ya hatari inayoweza kutokea endapo nchi zitaacha kuchukua hatua za kupambana na maambukizi na pia kwa sababuya kubanwa kijamii na kiuchumi.
Shirika la afya duniani WHO liliutangaza ugonjwa wa COVID -19 unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona kuwa ni dharura ya kimataifa mnamo mwezi Januari. Kamati ya asasi hiyo ya afya imesema inaendelea kulizingatia janga la corona kuwa bado ni hatari kubwa duniani. Mpaka sasa watu wapatao 680,000 wameshakufa duniani kote kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.Walioambukizwa wamefikia milioni 17.6 tangu ugonjwa huo uzuke mwaka uliopita katika jimbo la Wuhan la nchini China.
Nchi zimechukua hatua kali kwa lengo la kudhibiti maambukizi ambazo zimesababisha uchumi kudorora kwa kasi. Kamati ya shirika la WHO pia imetoa mwito wa kuunga mkono juhudi za kutoa tiba na chanjo zitakazothibitishwa kuwa salama. Kamati ya asasi ya WHO pia imewataka wadau waimarishe juhudi kwa lengo la kupata ufahamu mkubwa zaidi wa ugonjwa wa COVID -19 na athari zake za muda mrefu.
Mkurugugenzi mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema janga la corona litakuwapo kwa muda mrefu. Amekumbusha kuwa maradhi hayo yalipotangazwa kuwa janga la kimataifa, watu walioambukizwa hawakuzidi mia moja na hakuna waliokufa wakati huo nje ya China. Shirika la afya duniani limelaumiwa na Marekani kwa kuchelewa kuutangaza ugonjwa huo wa homa ya mapafu kuwa janga la kimataifa iliyodai kwamba shirika hilo linaegemea sana upande wa China. Marekani ilitangaza ilijiondoa rasmi kutoka kwenye shirika hilo mnamo mwezi wa Julai
Wakati huo huo watu zaidi ya 500,000 wameambulizwa virusi vya corona nchini Afrika Kusini na hivyo kuwa kitovu cha maambukizi hayo barani Afrika. Watu zaidi ya 8000 wameshakufa nchini humo. Hata hivyo watafiti wanahofia idadi hiyo huenda ikwa kubwa zaidi lakini Rais Cyril Ramaphosa amesema idadi ya vifo ni ya uwiano wa chini kabisa duniani. Afrika kusini inatambulika kuwa na mfumo wa afya imara kabisa barani Afrika lakini pana madai juu ya ufisadi. Rais Ramaphosa amewashutumu watu wanaojitajirisha kutokana na janga la corona.
Chanzo:/AFP