Wimbi la mauaji lazusha mashaka ya kiusalama Uganda
11 Juni 2018Kulingana na matamshi ya wanasiasa wa pande zote mbili pamoja na raia wa kawaida, sasa watu wote wana msimamo sawa kuhusu kile wanachoelezea kuwa kuzorota kwa usalama wa watu na mali zao.
Hivyo, mchanganyiko wa hisia za hamaki, huzuni na hofu kufuatia kifo cha mbunge huyo aliyeuawa kwa kupigwa risasa unadhihirisha kuwa wakati umewadia wa kuwepo na ushirikiano zaidi kukabiliana na visa vya mauaji ya kikatili ambavyo vimeshamiri kwa muda wa takriban miaka mitatu sasa.
Wakati jeneza la marehemu Ibrahim Abiriga lilipofikishwa kwenye majengo ya bunge, wengi wa wanasiasa walishindwa kudhibiti kuzuwia machozi yao.
Waliukubali ukweli kwamba mwenzao aliyefahamika kuwa mfuasi wa dhati wa chama tawala NRM na ambaye alikuwa mcheshi mwenye utu wa kiwango cha juu alikuwa hayupo tena.
Lakini mshtuko zaidi ni jinsi alivyouawa kinyama na kundi la watu wanaodaiwa walitoweka kwenye pikipiki zao mara tu baada ya kumumiminia risasa akiwa na ndugu yake wakielekea nyumbani kwao kufuturu kama ilivyo ada mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.
"Hivi vitendo tunavyoshuhudia vinatutia hofu ,hatujui nani anafuata Leo ni abiriga kesho hatujui ni nani tunaomba serikali ituisaidie kufuatia vizuri," alisema Taban Idd Amin ni mjukuu wa aliyekuwa rais wa Uganda ambaye pia ni mbunge wa Kiryandongo.
Tofauti za kimtazamo kuhusu wauaji
Huku rais Museveni akisema mauaji hayo yamefanywa na watu aliyowashtumu kuwa waasi wa ADF,wanasiasa wengine akiwemo mke wake mwenyewe Janet Kataha Museveni ambaye ni mbunge wa viti maalum na waziri, wametofautiana naye.
Wanasema kuwa pana haja serikali yake ichukue hatua madhubuti kukomesha mauaji ya aina hiyo kwani yanaelezea mengi kuhusu kiwango cha chuki na mgawanyiko miongoni mwa wananchi.
Wakati wa kuomboleza kifo cha marehemu Abiriga bungeni, Janet Museveni alisema: Tujiulize mauaji haya yana ujumbe gani kwa Waganda?Mbona kuna chuki kiasi hiki? Kifo cha Abiriga kiwe kioo kwetu kuzingatia chuki hii ambayo inasababisha vifo hivi vya kikatili nchini mwetu."
Mjini Arua kuliripotiwa machafuko huku wananchi wakionekana kuwa na hasira.Kanda za vijana wakivunjavunja viti vilivyoandaliwa kwa ajili ya shughuli za kuomboleza na mazishi zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Wanahoji kwa nini kwa muda mrefu serikali haijafanikiwa kukomesha mauaji ya kikatili yanayotendwa kwa njia hiyo hiyo ya watu wasiojuliakana wanaotoweka kwenye pikipiki baada ya kuwamiminia risasi wahanga wao.
Zaidi ya watu kumi mashuhuri wameauwa kwa namna hii katika kipindi cha miaka miwili. Lakini Kanali Felix Kulayigye mwakilishi wa majeshi bungeni amesema wauaji wanatumia ukatili ili kuwatishia Waganda na kuwafanya waichukie serikali yao.
Marehemu Abiriga atakumbukwa kwa ufuasi wake wa dhati kwa chama chake pamoja na utiifu wake kwa rais Museveni. Takriban kila kitu chake kuanzia mavazi, gari, vitu vya nyumbani ikiwemo malazi vilikuwa vya rangi ya manjano ambayo ni nembo ya chama tawala cha NRM.
Mwandishi: Lubega Emmanuel - DW Kampala.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman