1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa kutatuliwa mzozo wa Ethiopia waongezeka

1 Septemba 2021

Wasomi wa Afrika na wanaharakati ulimwenguni kote wamesaini barua ya wazi kwa Umoja wa Afrika wakitaka kuwepo upatanishi katika vita vya Ethiopia na kufanyika mazungumzo ya amani.

https://p.dw.com/p/3znHQ
Äthiopien Tigray-Krise | Soldaten TPLF
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Wachambuzi wamekubaliana kuhusu haja ya kuingilia kati na kumaliza umwagaji damu na kuzuia mzozo wa wakimbizi. 

Mamadou Diouf aliyesaini barua hiyo na profesa wa Masomo ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani, ameiambia DW kwamba kutokuwa na uwezo wa kuzuia mzozo huo ni kushindwa kwa Afrika nzima kwa ujumla.

Wito huo wa kupatikana amani bila shaka unaongeza wasiwasi kuhusu vita hivyo vinavyoingia mwezi wake wa tisa sasa bila ya kupatiwa suluhisho lolote.

Barua hiyo inasema "Ethiopia iko kwenye kingo" baada ya kulaani ukweli kwamba mzozo huo unaathiri idadi kubwa ya raia katika vita vinavyoelezwa kukiuka haki za binaadamu.

Äthiopien Bürgerkrieg Tigray
Mwanamke wa Tigray akisubiri kupewa msaada wa chakulaPicha: BAZ RATNER/REUTERS

Hassan Khannenje, mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati, anasema mzozo wa Tigray unazitia wasiwasi nchi nyingi za Afrika. Khannenje ameendelea kuorodhesha sababu kadhaa ikiwemo ukweli kuwa makao makuu ya Umoja wa Afrika yako mjini Addis Ababa na kwamba Ethiopia ni nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa kuwa na watu wengi.

"Kwa nchi kama Ethiopia yenye zaidi ya watu milioni 115, kusambaratika kwa nchi kutamaanisha kwamba dunia itakumbwa na mzozo wa wakimbizi ambao haijawahi kushuhudia katika historia ya hivi karibuni," alifafanua Khannenje.

Hili lina ukweli hasa kwa nchi jirani za Somalia na Kenya, ambazo zote zinapakana na Ethiopia. Nchi hiyo tayari imeyaondoa majeshi yake yaliyokuwa yakisaidia kupambana na magaidi wa al-Shabaab nchini Somalia.

Kuna hatari ya wakimbizi kufurika Kenya

Khannenje anasema kwa Kenya kuna hatari kubwa ya kufurika kwa wakimbizi katika kiwango ambacho pengine itashindwa kukimudu.

Akizidi kutengwa na washirika wake wa Magharibi, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed anatafuta uungaji mkono miongoni mwa mataifa ya Afrika. Siku ya Jumapili Abiy alikutana na Rais wa Rwanda Paul Kagame pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika ziara ya mara moja ya Kigali na Entebbe.

Amani na upatanishi vinaweza visiwe katika mawazo ya Abiy, lakini Khannenje anaamini kuwa anawategemea sana washirika wake wa kikanda na kijadi kujaribu kusaidia kwa upande wa kisiasa, lakini pia kwa kina kujaribu kupata silaha.

Äthiopien Ministerpräsident Abiy Ahmed trifft Ruandas und Ugandas Staatsoberhäupter
Abiy Ahmed alikutana na viongozi wa Uganda na Rwanda kuzungumzia masuala ya kikandaPicha: Lubega Emmanuel/DW

Abiy pia ameigeukia Uturuki kwa msaada. Michael Tanchum, mtafiti katika Taasisi ya Sera za Ulaya na Usalama ya nchini Austria, anasema Rais Recep Tayyip Erdogan anaiangalia Ethiopia kama msingi muhimu wa kutanua nyayo zake kiuchumi katika eneo kubwa la Afrika Mashariki hadi kusini kama ilivyofanya Kenya na Uganda.

Tanchum anasema Uturuki haiwazi tu kuhusu kuyafikia masoko na upatikanaji wa rasilimali, bali pia inataka kumaliza uwepo wa kimkakati wa Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu katika Pembe ya Afrika, kwa kuwa na uhusiano thabiti wa usalama na Somalia na Ethiopia.

Huku Uturuki ikiwa inaonekana kama kuigeukia Ethiopia, mshirika wa kijadi kwa ajili ya msaada wa kifedha na silaha za kijeshi, inazidi kuifanya hali ya kisiasa na kiusalama katika Pembe ya Afrika kuwa ngumu zaidi.

Mzozo wa Ethiopia na Sudan waongezeka 

Mzozo huo unazidi kuingia Sudan, ambako tayari kuna mvutano kuhusu ujenzi wa bwawa la umeme katika Mto Nile.

Kama ilivyo kwa Waafrika wengi, Mamadou Diouf ameiambia DW anaamini kwamba mzozo wa Tigray utatatuliwa na Waafrika wenyewe na hasa Umoja wa Afrika.

"Hatuwezi kuzibebesha nchi za Magharibi matatizo yetu. Hali hii inajitokeza sana Afrika, kwa sababu taasisi zetu hazifanyi majukumu yao ipasavyo," alisisitiza Diouf.

Wiki iliyopita Umoja wa Afrika ulimteua rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo kuwa mpatanishi. Nafasi yake ya kufikiwa kwa amani haionekani kuridhisha. Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF kinaushutumu Umoja wa Afrika kwa kumpendelea Abiy.

Mara kadhaa Abiy amekataa wito wa wajumbe wa ngazi ya juu kutoka Umoja wa Afrika kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Tigray. Anasisitiza kuwa mzozo huo ni suala la ndani. Khannenje anasema pande zote mbili zinaamini kuwa zinaweza kuwa na suluhusisho la kijeshi katika mzozo huo.

 

(DW)