Wito watolewa kukabili vifo vya wajawazito na watoto Afrika
29 Oktoba 2018Kongamano la pili la kimataifa barani Afrika limeanza leo mjini Nairobi nchini Kenya huku washirika wakiambiwa kuwa serikali za mataifa ya Afrika zinastahili kujitolea kwa hali na mali ili kukabiliana na vifo vya kina mama wajawazito na watoto ifikapo mwaka 2030. Kongamano hilo ambalo linahudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa 25 na washirika wapatao 1000, linajadili njia bora na salama za kina mama kujifungua.
Akifungua kongamano hili, mkewe rais Uhuru Kenyatta, Margaret Kenyatta alisema kuwa upo uwezekeno mkubwa wa kukabili vifo vya kina mama wajawazito na watoto ifikapo mwaka 2030 iwapo njia mbadala zitachangiwa na waafrika wenyewe. Kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa nchini Kenya, watoto 22 hufariki dunia kabla ya kufikisha mwezi mmoja huku 193,000 wakizaliwa kabla ya siku zao.
Bi uhuru Kenyatta ameendelea kusema:
"Kauli mbiu ya leo inakwenda sambamba na mikakati yangu ya kupunguza idadi ya viifo kwa wanawake waojifungua na kila mtoto anastahili kuishi zaidi ya miaka mitano.. Ni vita ambavyo nimekuwa nikipigana navyo kwa muda wa miaka mitano sasa, na leo naongezea sauti yangu kwenye vita hivi naamini kuwa kila mama na kila mtoto anastahili kuishi na kushamiri.”
Serikali ya Uingereza imetoa dola milioni 15 kwa ajili ya mpango wa kupunguza vifo vya kina mama wanaojifungua nchini kenya.
Wanawake 550 hufariki kila siku kutokana na matatizo ya ujauzito
Kongamano hili la pili linafuatia lile ambalo lilifanyika Afrika Kusini miaka mitano iliyopita, huku wanawake 550 wakiripotiwa kufa kila siku kutokana na matatizo ya ujauzito katika mataifa yaliyoko chini ya jangwa la sahara. Kenya imetajwa kuwa mfano kwa mataifa mengine ya Afrika huku mfumo wa ugatuzi ukichangia kuboresha sekta ya afya mashinani hasa katika majimbo yaliyoko kaskazini ambayo yalikuwa na viwango vikubwa vya vifo vya kina mama wajawazito na watoto kutokana na uhaba wa vifaa. Mratibu wa Umoja wa Mataifa daktari Siddharth Chatterjee anasema:
"Ni kwa sababu ya uongozi wa kitaifa na majimbo, rais Uhuru Kenyatta, baraza lake la mawaziri na magavana wa majimbo. Kwa hivyo pana haja ya kuwa na nia njema ya kisiasa.”
Chaterjee anaongeza kusema kuwa pana haja ya mataifa ya Afrika kutafuta suluhisho kwa matatizo yanayolikumba bara hili badala ya kusubiri mataifa wafadhili iwapo malengo ya afya kwa wote yataafikiwa.
Hamasisho la kupunguza vifo
Tume ya ya Umoja wa Afrika ambayo inafadhili kongamano hili pamoja na serikali ya Kenya imesema kuwa inashirikiana na benki ya dunia, benki ya maendeleo barani Afrika na Shirika la Chakula Ulimwenguni pamoja na wake wa marais wa bara la Afrika kuhamasisha wananchi wa mataifa husika ili kupunguza vifo hivyo. Bibi Amira Elfadil ni msimamizi wa masuala ya kijamii katika Tume ya Umoja wa Afrika. "Nina uhakika kuwa tukiafikia malengo ya maendeleo endelevu ya millennia kuhusu Afya ifikapo mwaka 2030, tutakuwa na raia wenye afya bora na watachangia Afrika kutimiza malengo yake.”
Kando kando ya mkutano huu, kuna vibanda vya teknolojia vainavyonyesha njia mbadala ya kukabiliana na ongezeko la vifo vya kina mama wajawazito na watoto. Ahmed Nadhir ni waziri wa afya wa jimbo la Garissa kwenye moja ya vibanda hivi.
Kongamano hili la siku tatu litajadili masuala mengine yakiwemo, uongozi uajibikaji, virusi visababishavyo Ukimwi miongoni mwa watoto pamoja na ndoa na mimba za mapema.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman