Xi Jinping ziarani Korea Kaskazini
20 Juni 2019Pasipo kutoa maelezo ya kina shirikia la habari la China Xinhua limesema Rais Xi Jinping na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wamekutana kwa mazungumzo mjini Pyongyang. Awali Xi na mkewe Peng Liyuan na maafisa waandamizi wa China walikaribishwa kwa mizinga 21, katika gwaride kubwa la heshima lililofanyika katika uwanja wa ndege wa Pyongyang.
Takribani watu 10,000 walijipanga vyema, huku wakipunga maua hewani na kuimba kwa sauti karibu Xi, karibu Xi. Kim na mkewe Ri Sol Ju, walikutana na ujumbe wa wapokeaji kwenye uwanja wa ndege huo. Xi yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Korea Kaskazini, ambapo inaelezwa kuwa ni ziara ya kwanza kwa kiongozi wa china kuwasili nchini humo katika kipindi cha miaka 14.
Migogoro ya Korea Kaskazini na China
Mkutano huo unafanyika wakati Xi na Kim wanakabiliwa na migogoro tofauti na Marekani. Xi wa kibiashara na Kim kuhusu silaha za nyuklia. Kwa mujibu wa Xinhua China inaweza kucheza karata ya kipekee na ya kujijenga kwa kuondosha hali ya kutoaminiana kati ya Korea Kaskazini na Marekani ili waweze kufanya kazi pamoja kufanikisha jitihada za kuondosha matumizi ya nyuklia.
Marekani inaitaka Korea Kaskazini kuachana na kuendeleza silaha za nyuklia kabla ya kuondoshewa vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa taifa hilo. Lakini Korea Kaskazini imetaka muda wa hatua kwa hatua katika kulitekeleza hilo, huku ikihimiza kupata unafuu wa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa. Katika suala hilo China inataka uwiano sawa wa kila upande na si kuwepo kwa shinikizo la upande mmoja na matakwa yasio akisi hali halisi.
Mwanadiplomasia wa zamani wa Korea Kaskazini Thae Yong Ho aliyetoroka mwaka 2016 anasema, anadhani Kim anataka kumpa ujumbe Xi wa kuuwakilisha kwa Rais Trump, pale ambapo viongozi hao wawili watakapokutana katika mkutano wa kilele wa mataifa ya nchi za G20 wa juma lijalo unaotarajiwa kufanyika nchini Japan.
Lakini pia alionya kuwa hatua ya namna hiyo inaweza kuwa ya kuvuta muda tu na sio kuachana na matumizi ya nyuklia.
Mazungumzo ya Marekani na Korea Kaskazini yamekwama tangu Kim na Trump wafanye mkutano wao wa kilele wa mara ya pili Februari mjini Hanoi, Vietnam.
Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri: Yusuf Saumu