YANGON : Jeshi lazidi kukandamiza upinzani
27 Septemba 2007Vikosi vya utawala wa kijeshi wa Burma vimeusafisha mji mkuu wa Yangon kwa kuwaonya waandamanaji kwa hatua kali kuwatia mbaroni mamia na kufyetuwa risasi za moto hewani.
Watu tisa wameuwawa kwa kupigwa risasi akiwemo mwandishi habari wa Japani.Umma ulitawanyika lakini kumekuwepo na repoti kwamba baadhi yao wameendelea kukaidi amri ya serikali ya kurudi majumbani.Wakati wa usiku jeshi lilivamia nyumba za watawa wa kibuda na kuwasomba mamia ya mabuda ambao ndio walioongoza maandamano hayo yaliochochewa na kupanda kwa bei ya mafuta.
Bunge la Umoja wa Umoja wa Ulaya limetowa wito kwa Umoja wa Ulaya,Marekani na nchi za kusini mashariki ya Asia kuwawekea vikwazo viongozi wa kijeshi wa Burma na kuitaka Cahina na Urusi kujiunga na nchi nyengine wanachama wa Baraza la Usalama kwa kulaani ukandamizaji huo.
China ambayo ni mshirika wa utawala wa kijeshi nchini Burma imepinga matumizi ya vikwazo dhidi ya nchi hiyo na imetaka wahusika wote nchini Burma kujizuwiya kuchukuwa hatua za kuuchochea mzozo huo.