YANGON: Mjumbe wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa awasili Myanmar
11 Novemba 2007Mjumbe wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Paulo Sergio Pinheiro, amewasili nchini Myanmar kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Katika ziara yake ya siku tano, na ambayo pia ya kwanza katika kipindi cha miaka minne, mjumbe huyo atachunguza matumizi ya nguvu kupita kiasi katika kuyazima maandamano ya kupigania demokrasia yaliyoongozwa na watawa wa kibuda mnamo mwezi Septemba mwaka huu.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva nchini Uswisi, wamesema Paulo Sergio Pinheiro amewasilisha orodha ya magereza na vituo vya kuwazuilia wafungwa anavyotaka kuvitemvbelea wakati wa ziara yake nchini Myanmar.
Mpambe wa mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema utawala wa kijeshi nchini Myanmar umeashiria uko tayari kushirikiana naye.
Ziara ya Paulo Sergio Pinheiro inafanyika siku mbili baada ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeushulikia mzozo wa Myanmar, Ibrahim Gambari, kuondoka mjini Yangon baada ya kufanya ziara ya siku sita.
Ziara ya kiongozi huyo imeleta matumaini makubwa kwamba jeshi la Myanmar litakuwa tayari kushiriki kwenye mazungumzo juu ya mageuzi ya kisiasa pamoja na kiongozi wa upinzani nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi.